“Dunia inapoteza kiwango kikubwa sana cha chakula,” ndivyo ilivyoanza video ya ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika siku hii iliyotengwa maalum kukumbusha umuhimu wa kufanya manunuzi na kutumia chakula kwa kiwango kinachotosheleza bila kutengeneza taka.

Akitoa takwimu za ukubwa wa changamoto hiyo, Guterres amesema  “kila siku, tunatupa chakula kinachoweza kuandaa milo bilioni 1 huku tukiruhusu asilimia 9 ya watu duniani kubaki na njaa. Tunaiweka hatarini tabianchi, mifumo ya ikolojia na afya yzetu binadamu, pamoja na kudhoofisha uwezo wetu kujilisha katika siku zijazo.”

Anasema katika jamii kila mtu ana jukumu la kufanya ili kutozalisha taka.

“Watumiaji, wanaweza kuchangia kwa kufanya mabadiliko madogo katika namna wanavyonunua na kupika. Wafanyabiashara, wanaweza kuboresha mifumo yao ya usambazaji na kusambaza upya chakula kinachobaki. Miji, inaweza kupanua utenganishaji wa taka asilia na kuimarisha ununuzi wa chakula kwa taasisi kama shule na hospitali. Na serikali za kitaifa, zinaweza kuleta mabadiliko ya kimfumo kwa kushughulikia upotevu wa chakula katika mipango yao ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na uhifadhi wa bayonuai, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.”

Akiunga mkono ushauri huo, Nabil Gangi, ambaye ni Mratibu wa Kanda Ndogo ya Asia ya Kati na Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO nchini Uturuki amesema. 

“Ningependa kuwakumbusha wote kwamba kuzuia upotevu wa rasilimali ni jambo tunaloweza kufanya kila siku. Sio tu kama wazalishaji, wasafirishaji au wauzaji wa bidhaa, bali pia kama watumiaji,iwe ni kwa kupanga vizuri orodha ya manunuzi, kuhifadhi chakula kwa njia sahihi, kuchagua bidhaa zinazoweza kutumika tena, au kuunga mkono biashara zinazopunguza upotevu na kutangaza juhudi hizo. Kila chaguo tunalofanya husaidia kulinda mazingira yetu na kuhakikisha chakula kinaishia mezani, siyo kwenye mapipa ya taka.” 

Kuna mipango ya kimataifa kama ‘Mapinduzi ya Upotevu wa Chakula’ na ‘Kutozalisha taka asilia’ iliyoanzishwa katika mkutano wa mabadiliko ya tabianchi wa COP30 ambayo inalenga kupunguza nusu ya upotevu wa chakula ifikapo mwaka 2030, kupunguza uzalishaji wa gesi ya methani kwa hadi asilimia saba, na kujenga mifumo imara na endelevu ya chakula.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *