Katika kikao maalum cha Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa ECOSOC, uliofanyika mjini New York, Umoja wa Mataifa umetaka mageuzi ya haraka katika mfumo wa kimataifa wa viwango vya mikopo, ukionya kuwa mfumo huo unazikwamisha nchi zinazoendelea.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu António Guterres, Naibu Katibu Mkuu Amina J. Mohammed amesema huu ni mkutano wa kwanza unaokutanisha serikali, wawekezaji na taasisi za kutoa viwango vya mikopo kushughulikia changamoto hiyo kwa pamoja.

Madeni yanayoongezeka sanjari na shinikizo

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wameonya kuwa upatikanaji wa fedha “mafuta ya maendeleo endelevu” unaendelea kupungua huku gharama za kukopa zikiongezeka.

Nchi zinazoendelea sasa zinatumia karibu dola trilioni 1.4 kila mwaka kulipa madeni, huku zaidi ya watu bilioni 3.4 wakiishi katika nchi zinazotumia fedha nyingi kulipa riba kuliko afya au elimu.

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umeonya kwamba mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati umeongeza shinikizo katika uchumi wa dunia kwa kupandisha bei za mafuta na bidhaa ghafi.

Viwango vya mikopo vyalaumiwa ni vya hatari kupita kiasi

Moja ya hoja kuu katika mkutano wa leo ECOSOC ni nafasi ya taasisi za viwango vya mikopo katika kuzuia upatikanaji wa fedha.

Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, tathmini za sasa mara nyingi hutegemea mitazamo ya muda mfupi na taarifa zisizo kamili, hivyo kuonesha picha mbaya zaidi ya hali halisi ya uchumi wa nchi zinazoendelea. “Viwango vya mikopo vinapaswa kufungua milango ya ufadhili wa muda mrefu,” amesema Bi. Mohammed, “lakini mara nyingi vinazuia nchi kupata mikopo nafuu licha ya uwezo wao wa muda mrefu wa kukua.”

UN yapendekeza ramani ya mageuzi

Kwa kujenga juu ya makubaliano ya kimataifa kama Mkataba wa Zama Zijazo na mkutano wa Sevilla, Umoja wa Mataifa umependekeza hatua kadhaa za kurekebisha mfumo wa kifedha wa kimataifa.

Hatua hizo ni pamoja na kuanzisha jukwaa la wakopaji ili kuzipa nchi zinazoendelea sauti kubwa zaidi, kuweka kanuni za ukopaji na ukopeshaji wenye uwajibikaji, na kuwakutanisha wadau kubuni mfumo wa madeni unaolenga maendeleo.

Pendekezo la kuanzishwa kwa Wakala wa Viwango vya Mikopo wa Afrika limetajwa kama hatua muhimu ya kuongeza uwazi na takwimu bora.

Wito wa uwazi, uwajibikaji na mtazamo wa muda mrefu

Umoja wa Mataifa umesisitiza misingi mitatu ya mageuziambazo ni, kuhama kutoka tathmini za muda mfupi kwenda uwekezaji wa muda mrefu, kutambua faida za maendeleo kupitia mikopo yenye uwajibikaji, na kuimarisha uwajibikaji kwa serikali, wawekezaji na taasisi za viwango vya mikopo.

Mohammed alisisitiza kuwa tathmini za kifedha zinapaswa kwenda zaidi ya Pato la Taifa GDP na kujumuisha maendeleo ya kijamii na kimazingira.

“Ni wakati wa kubadili viwango vya mikopo kutoka kuwa vizuizi hadi kuwa chachu ya maendeleo endelevu,” amesema, akitoa wito wa ushirikiano wa kimataifa kuhakikisha nchi zinazoendelea zinapata fedha nafuu kwa maendeleo yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *