
Serikali ya Uispania imetangaza kufunga anga ya nchi hiyo kwa ndege zote za kijeshi zinazohusiana na mashambulizi dhidi ya Iran, kama ishara ya kupinga vita vinavyoongozwa na Marekani na Israel.
Waziri wa Ulinzi wa Uhispania, Margarita Robles, alisema siku ya Jumatatu: “Ni wazi kwamba anga ya Uhispania hairuhusiwi kutumika kwa shughuli zozote zinazohusiana na vita dhidi ya Iran.”
Naye Carlos Cuerpo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Uchumi, amesitiza kuwa hatua hiyo ni “sehemu ya uamuzi wa serikali ya Uhispania wa kutoshiriki wala kuunga mkono vita hivyo vya upande mmoja ambayvyo vinakiuka sheria za kimataifa.”
Kwa mujibu wa gazeti la Kihispania la El País, marufuku hiyo inakwenda mbali zaidi ya vizuizi vilivyokuwepo awali kuhusu kuruhusu ndege kuruka kutoka vituo vya kijeshi vya Uhispania vya Rota na Morón kwa ajili ya mashambulizi au kujaza mafuta angani. Sasa pia inahusu ndege za kijeshi zinazotoka katika vituo vya Uingereza, Ufaransa na nchi nyingine. Gazeti hilo liliongeza kuwa ruhusa maalumu inaweza kutolewa tu katika hali za dharura.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa Madrid imekuwa miongoni mwa wakosoaji wakubwa barani Ulaya wa vita dhidi ya Iran ambavyo vinaendelezwa na Marekani na Israel. Tangu kuanza kwa vita , Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sánchez amesisitiza mara kadhaa kauli mbiu ya “Hapana kwa vita!”
Takribani mwezi mmoja uliopita, muda mfupi baada ya kuanza kwa vita tarehe 28 Februari, Sánchez alipiga marufuku matumizi ya vituo vya kijeshi vya Rota na Morón na majeshi ya Marekani kwa operesheni dhidi ya Iran. Vituo hivyo vilivyoko Andalusia kusini mwa Uhispania vimekuwa vikisimamiwa kwa pamoja na Uhispania na Marekani kwa miongo kadhaa.
Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa msimamo wa Sánchez una mizizi ya kisiasa ya ndani. Kwa muda mrefu, jamii ya Uhispania imeonyesha mashaka makubwa kuhusu uingiliaji wa kijeshi wa Marekani na Israel. Wakati wa vita vya Gaza, mamia ya maelfu ya Wahispania walifanya maandamano ya kuunga mkono Palestina.
Kwa mujibu wa televisheni ya Austria, Sánchez pia ameishutumu Israel kwa kufanya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza. Baada ya hapo, Uhispania ilisimamisha usafirishaji wa silaha kwenda Israel, ikamwita balozi wake kutoka Tel Aviv, na ikatambua rasmi dola la Palestina. Aidha, Uhispania imekosoa vikali ushiriki wa Israel katika mashindano ya muziki ya Eurovision yaliyofanyika Vienna.
Waziri Mkuu Sánchez pia amekumbusha matokeo ya vita vya Marekani dhidi ya Iraq na kusema: “Miaka ishirini na tatu iliyopita, serikali nyingine ya Marekani ilituingiza katika vita vya Mashariki ya Kati.” Amesema vita vya Iraq havikutoa matokeo yaliyokuwa yameahidiwa wakati huo. Pia alimshutumu Donald Trump kwa “kucheza kamari hatari na hatima ya mamilioni ya watu.”