
Tovuti ya CNBC imeandika kwamba uungaji mkono wa vikosi vya Yemen kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mashambulizo ya kichokozi ya Marekani na Israel dhidi yake na urushaji wa makombora wa Wayemen kuelekea Palestina inayokaliwa kwa mabavu umepelekea bei ya mafuta kuongezeka sana katika soko la kimataifa.
Tovuti ya CNBC imesema: Bei ya mafuta yasiyosafishwa ya Brent iliongezeka mapema Jumatatu asubuhi kwa dola 2.47 na kufikia dola 115.35 kwa pipa. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mafuta ghafi ya West Texas Intermediate pia yalipanda bei kwa asilimia 1.62 hadi $101.25 kwa pipa.
David Roche, mwanamkakati wa shirika la Quantum Strategy, ameiambia CNBC kwamba kuendelea kwa mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran na kulipiza kisasi kwa Tehran kunaweza kuathiri haraka njia za usambazaji mafuta duniani, akionya kwamba bomba la mafuta la Saudi Arabia la Mashariki-Magharibi, ambalo hubeba takriban mapipa milioni 5 ya mafuta kwa siku hadi Bahari Nyekundu, liko hatarini na kwamba uvurugaji wowote katika usafirishaji wa mafuta kupitia Lango Bahari la Bab al-Mandab unaweza kuwa na taathira kubwa. Kuhusiana na suala hilo, taasisi ya Uingereza ya Chatham House, imekiri kuhusu uwezo wa jeshi la Ansarullah la Yemen wa kuvuruga mzunguko wa uchumi wa dunia iwapo litavuruga shughuli za uchukuzi katika Lango-Bahari la Bab al-Mandab na Bahari Nyekundu.