
Dodoma. Spika wa Bunge, Mussa Zungu ameziweka kwenye mabano halmashauri za wilaya ambazo hazikuchukua dawa za kuua viluilui vya mazalia ya mbu katika kiwanda cha Kibaha.
Zungu ametoa maagizo hayo leo Alhamisi Aprili 2,2026 wakati wa kuhitimisha kipindi cha ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu.
“Serikali naomba mpokee maagizo ya kiti, nataka mlete orodha ya halmashauri zote ambazo zilikaidi kuchukua dawa hizo na orodha ifike ofisini kwa Katibu wa Bunge ifikapo Aprili 8,2026 mchana na hatua zilizochukuliwa kwa watu hao,” amesema Zungu.
Awali Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Rose Tweve amemuuliza Waziri Mkuu kuwa, ni kwa nini baadhi ya halmashauri hazikuchukua dawa hizo ambalo ni agizo la Serikali kwa ajili ya kuwa viluilui vya mbu.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, hivi karibuni Kamati yetu ilitembelea kiwanda kikubwa cha kuzalisha dawa za kuua mazalia ya mbu, lakini tulikuta lundo la dawa na halmashauri nyingi wanasema hazikuchukua, nataka kujua tatizo ni nini na hatua gani zitachukuliwa kwa wahusika,” ameuliza Tweve.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amekiri ni kweli kumekuwa na agizo la Serikali kwamba halmashauri zote zichukue dawa hizo lakini pia watumishi wake wanahitaji kupatiwa mafunzo.
Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi afuatilie tatizo hilo kwa haraka na hadi ifikapo Mei mwaka huu wahusika wawe wamechukua na wapatiwe mafunzo.
Dk Mwigulu amefafanu kuwa mara nyingi maagizo ya mafunzo kwa watumishi hutakiwa yafanyike Juni kipindi ambacho maeneo mengi nchini huwa hakuna mvua.
Wakati huohuo Waziri Mkuu amesema zinatakiwa Sh1 trilioni ili kukabiliana na wimbi kubwa la wanafunzi ambao ni zaidi ya milioni tatu watakaojiunga kidato cha kwanza 2028.
Fedha hizo zinakadiriwa kujenga zaidi ya madarasa 23,200 na maabara 9,300 lakini lengo ni kujenga madarasa matatu ya sekondari kwa kuanzia katika kila kijiji.
Ametoa majibu hayo kufuatia swali la Mbunge wa Mbarali (CCM) Bahati Ndingo ambaye ametaka kujua ni mkakati gani wa Serikali uliowekwa kama maandalizi ya kupokea wanafunzi wa madarasa ya saba na sita 2027 ambao kwa pamoja watafanya mtihani wa kuhitimu na kujiunga na sekondari.
Hata hivyo, jana wakati anasoma hotuba ya wizara yake na zilizo chini yake Dk Mwigulu alitaja mkakati mwingine ni kuongeza ajira za walimu zaidi ya 40,000 ambao umeshaanza kutekelezwa mwaka huu.