Morogoro. Wakulima wa mpunga wanaotegemea mvua nchini wameeleza namna watafiti wa Mradi wa Mpunga Himilivu kwa Mabadiliko ya Tabianchi na Rafiki kwa Mazingira barani Afrika (CERA) walivyowasaidia kwa kuzalisha mbegu bora zinazostahimili ukame na changamoto za hali ya hewa.

Hatua hiyo imeelezwa kusaidia kuongeza uzalishaji na kipato cha wakulima licha ya mabadiliko ya tabianchi. Akizungumza na wakulima wa Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro, Mtafiti Mkuu wa mradi huo, Profesa Suzan Msolla kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo amesema lengo ni kuimarisha ustahimilivu wa zao la mpunga dhidi ya ukame.

Amesema mradi huo unalenga kuwasaidia wakulima wa Tanzania na Kenya kukabiliana na changamoto za hali ya hewa huku ukipunguza pengo la kijinsia kwa kuwawezesha zaidi wanawake wanaoongoza kaya. Pia unahusisha uendelezaji wa mbegu bora zinazokidhi mazingira ya ndani na zinazopendwa na wakulima.

Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya utafiti wa Kilimo Tanzania TARI Dkt. Atugonza Bilaro akizungumza na wakulima wa mpunga wa wilaya ya Kilosa wanaolima kwa kutegemea mvua. Picha Hamida Shariff

Profesa Msolla ameongeza kuwa watafiti wanatekeleza mbinu bora za kilimo katika maeneo yenye ukame, ikiwemo upandaji wa moja kwa moja na kilimo cha mzunguko, ili kupunguza matumizi ya maji na kulinda mazingira. Aidha, uwezo wa taasisi za ndani utaimarishwa kupitia mafunzo na uwekezaji katika miundombinu ya utafiti.

Kwa upande wao, wakulima kutoka Morogoro, Shinyanga na Songwe wamesema mradi huo ni matumaini mapya. Mkulima wa Kijiji cha Shilela, Wilaya ya Mlele, Maroja Shana amesema mvua zimekuwa hazitabiriki, jambo linalosababisha upungufu wa maji mashambani na kupunguza mavuno.

Naye Zilpa Simchimba kutoka Momba, Songwe amesema ukame unaathiri zaidi wanawake wanaobeba jukumu la familia, hali inayowalazimu kupunguza milo au kuuza mazao kidogo wanayopata ili kukidhi mahitaji muhimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *