
Dar es Salaam. Wakati mataifa mengi yakikumbwa na athari za mapigano yanayoendelea Mashariki ya Kati, Tanzania imeanza kunufaika na mabadiliko ya mwenendo wa uwekezaji duniani, hasa katika sekta ya viwanda vya magari yanayotumia nishati safi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, leo Aprili 2, 2026 alipokuwa akitoa taarifa ya uwekezaji, Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (Tiseza), Gilead Teri amesema mabadiliko hayo yamesababishwa na kupanda kwa gharama za uzalishaji, kuvurugika kwa minyororo ya usambazaji na changamoto za kiusalama katika baadhi ya maeneo.
Ametoa kauli hiyo wakati akiwasilisha hali ya uwekezaji katika robo ya kwanza ya mwaka 2026 (Januari hadi Machi).
Amesema katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu, maombi matano tayari yamewasilishwa Tiseza yakionyesha nia ya kuanzisha viwanda vya kutengeneza magari yanayotumia umeme na betri nchini.
“Hii inaonyesha mwelekeo mpya wa uwekezaji katika nishati safi na teknolojia rafiki kwa mazingira. Tunaona wazi Tanzania inaanza kuwa kitovu cha uwekezaji katika sekta hii ndani ya ukanda,” amesema.
Amesema mapigano yanayoendelea Mashariki ya Kati yameanza kuleta athari chanya kwa Tanzania, kwani wawekezaji wengi sasa wanatafuta maeneo mbadala yenye utulivu. Tanzania imekuwa chaguo muhimu kutokana na mazingira yake rafiki ya uwekezaji,” amesema Teri.
Katika kipindi cha Januari hadi Machi 2026, Tiseza imesajili miradi 177 ambayo inategemea kuwekeza mtaji wa Dola za Marekani 1.122.09 bilioni (Sh2.91 trilioni) na kuzalisha ajira 19,750 katika sekta mbalimbali nchini.
Sekta ya uzalishaji viwandani imeendelea kuongoza katika usajili wa miradi kwa asilimia 51, idadi ya ajira zitakazo zalishwa kwa asilimia 63 na kwa mtaji utakao wekezwa kwa asilimia 47.
Teri amesema sekta tano zinazoongoza kwa uwekezaji nchini ni uzalishaji wa viwandani, utalii, majengo ya biashara/ujenzi, miundombinu ya uchumi na kilimo.
“Sekta hizi ni za kimkakati ambazo zina machango zaidi katika maendeleo ya nchi kwa kuleta fedha za kigeni, kuchagia katika pato la Taifa, kutoa ajira nyingi zaidi,” amesema.
Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani bado imeendelea kuwa kinara wa kuvutia uwekezaji na kutoa ajira kutokana na kuwepo kwa miundombinu wezeshi kama barabara, umeme, maji, reli na karibu na bandari.
“Tiseza itaendelea kuweka mazingira bora kwa kuweka mazingira bora kwa mikoa ambayo ipo pembezoni kwa kuwa na vivutio maalum vya kikodi na visivyo vya kikodi ambavyo vitawashawishi wawekezaji kwenda kuweza huko,” amesema.
“Hadi kufikia Aprili Mosi, 2026, mamlaka imepokea jumla ya maombi ya wawekezaji 86 walioonesha nia ya kuwekeza katika maeneo hayo, ambapo kwa mchanganuo ni Bagamoyo (48), Kwala (20), Nala (16) na
Buzwagi (2),”
“Kutokana na jitihada za kutangaza maeneo haya ndani na nje ya nchi, Tiseza imefanikiwa kusaini mikataba ya ardhi na kampuni 27 sawa na asilimia 31 ya maombi,”.
Amesema miradi hii inategemea kuwekeza zaidi Sh177 bilioni na kuzalisha ajira zaidi ya 4,140 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
“Bagamoyo inakwenda kuwa eneo la kimkakati si tu kwa viwanda, bali pia kwa usafirishaji wa mizigo kupitia bandari inayotarajiwa kujengwa,” amesema.
Kuhusu fidia kwa wakazi, amesema mchakato unaendelea na wananchi wanahimizwa kuhakiki taarifa zao ili waweze kulipwa kwa wakati.
“Uwekezaji unakuja, viwanda vinajengwa na maeneo haya yanahitajika. Tunahakikisha kila mwenye stahiki anapata fidia yake,” amesema.