Dar es Salaam. Jumla ya wanafunzi 561 wamewasilisha maandiko ya ubunifu kuhusu utatuzi wa changamoto ya msongamano wa magari mijini.

Lengo la shindano hilo lililoanza Machi 3, 2026 na kuhitimishwa Machi 31, lilikuwa ni kuwapa ushiriki thabiti na kuibua fikra bunifu miongoni mwa wanavyuo na watalaamu wachanga.

Kwa mujibu wa Wizara ya Ujenzi, lengo jingine la shindano hilo lililopewa jina la Ubunifu kwa Wanafunzi Challenge, lilikuwa kuwahamasisha waweze kuhusianisha ujuzi wanaoupata kupitia masomo yao vyuoni na changamoto zilizopo katika jamii.

Baada ya mchakato huo kufungwa, kinachosuburiwa kwa sasa ni maandiko hayo kuchakatwa, kupitia kamati ya wataalamu 13 walioteuliwa na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega.

Akizungumza na wanahabari leo Alhamisi, Aprili 2, 2026 Waziri Ulega amesema chemsha bongo hiyo ilipokewa vizuri na Watanzania na wanataaluma hao wa uhandisi walipata mwitikio mkubwa.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu shindano la ubunifu linalohusisha wanafunzi wa uhandisi kubuni mikakati ya kumaliza tatizo la msongamano wa magari kwenye miji mikubwa nchini Tanzania, jana.

“Nawashukuru pia Watanzania wengine waliotufuata kututia moyo, kuboresha na kutoa maoni yao kuhusu namna sisi wenyewe tunavyoweza kukabili changamoto zetu,” amesema Ulega.

Hata hivyo, Ulega amesema licha ya shindano hilo kuwa mahususi kwa ajili ya wanafunzi, wizara ilipokea maoni na mawasilisho mengi kutoka kwa vijana wa Kitanzania ndani na nje ya nchi ambao si wanafunzi.

“Kufuatia wingi wa maombi, nimeunda jopo la wataalamu lenye wajumbe 13 ili kufanya tathmini ya maandiko yaliyowasilishwa.

“Katika kamati hii nimejumuisha wajumbe kutoka taasisi mbalimbali za umma na binafsi, pamoja na vyama vya wadau wa usafirishaji,” ameeleza Ulega.

Kwa mujibu wa Ulega, kamati hiyo itakuwa na majukumu saba likiwemo la kupokea mawasilisho kutoka kwa washiriki, kutambua malengo na miongozo ya shindano na kuandaa vigezo vya ubora.

Mengine ni kutathmini mawasilisho kulingana na vigezo vilivyoidhinishwa, kupendekeza washindi, kuandaa wasilisho la mapendekezo kwa wakuu wa taasisi na kuandaa taarifa ya Washindi.

“Baada ya kamati kukamilisha uchambuzi wa kina, watawasilisha taarifa na mapendekezo yao kwa majaji wa shindano ambao ni wakuu wa taasisi zote zilizoko chini ya Wizara ya Ujenzi,”

“Majaji watapokea taarifa ya tathimini kutoka kwa kamati na kuwafanyia mahojiano washindi kabla ya mchakato kukamilika na hatimaye kuwapata washindi, watakaopewa zawadi Aprili 30,” amesema.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu shindano la ubunifu linalohusisha wanafunzi wa uhandisi kubuni mikakati ya kumaliza tatizo la msongamano wa magari kwenye miji mikubwa nchini Tanzania, jana.

Zawadi zaongezwa

Ulega amesema awali walitangaza zawadi ya Sh10 milioni ambayo ingegawanywa kwa washindi watatu wa mwanzo, lakini kutokana na mwitiko chanya wa Watanzania, wadau wa sekta ya ujenzi na taasisi zake wameongeza zawadi hiyo.

Kutokana na nyongeza hiyo, Ulega amesema kwa sasa mshindi wa kwanza atajinyakulia Sh10 milioni, wa pili (Sh5 milioni), wa tatu (Sh3 milioni), wa nne (Sh2 milioni) na watano hadi saba wapata Sh1 milioni.

 “Mshindi wa nane hadi wa 10 atapata Sh500, 000 kila mmoja. Mbali na zawadi hizo, washindi watapewa kompyuta mpakato na kutafutiwa sehemu za kuongeza ujuzi katika makampuni mbalimbali nchini watakapomaliza masomo yao,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *