Russia. Machi 30, 2026, dunia iliadhimisha Siku ya Kimataifa ya Ugonjwa wa Akili ujulikanao kama Bipolar, siku inayolenga kuongeza uelewa kwa jamii, kupunguza unyanyapaa na ubaguzi pamoja na kuhimiza upatikanaji wa huduma za afya ya akili.

Siku hii huchaguliwa kwa heshima ya siku ya kuzaliwa ya msanii maarufu wa Uholanzi, Vincent van Gogh, ambaye alihusishwa na ugonjwa huo baada ya kifo chake.

Bipolar au Baipola kwa Kiswahili, ni hali ya afya ya akili inayosababisha mabadiliko makubwa ya hisia. Mabadiliko hayo hujumuisha vipindi vya furaha iliyopitiliza na huzuni kali, hali inayoweza kuathiri maisha ya mhusika kwa kiasi kikubwa.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani  (WHO), takribani watu milioni 40 duniani wanaishi na ugonjwa huu, huku tafiti zikionesha kuwa waathirika wanaweza kufariki mapema kwa wastani wa miaka 10 ikilinganishwa na watu wengine.

Wagonjwa wa Bipolar hukumbana na changamoto nyingi, hasa katika jamii zenye uelewa mdogo wa afya ya akili. Unyanyapaa, ubaguzi na kutengwa na familia au jamii ni baadhi ya matatizo yanayowakabili.

Bila matibabu sahihi, dalili za ugonjwa huu huweza kumfanya mhusika kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kila siku ikiwamo kusoma na kufanya kazi.

Hadi sasa, wataalamu wa afya ya akili hawajabaini sababu ya moja kwa moja ya ugonjwa huu, lakini wanaeleza kuwa unatokana na mchanganyiko wa sababu mbalimbali kama vile urithi wa kijenetiki, muundo wa ubongo, msongo wa mawazo na mazingira ya maisha. Sababu hizi huathiri mfumo wa fahamu, nguvu ya mwili na uwezo wa kufikiri.

Dalili za Bipolar mara nyingi huanza kujitokeza wakati wa ujana au utu uzima wa mapema, ambapo idadi kubwa ya wagonjwa hupata dalili kabla ya kufikisha miaka 25.

 Ugonjwa huu hujitokeza katika vipindi vya hali ya juu ambapo mhusika anaweza kuwa na furaha isiyo ya kawaida, nguvu nyingi, kuongea haraka, kukosa usingizi na kufanya uamuzi wa hatari.

 Pia hujitokeza katika vipindi vya hali ya chini vinavyoambatana na huzuni kali, kukosa matumaini, uchovu, mabadiliko ya usingizi, kujitenga na wakati mwingine kuwa na mawazo ya kujiua.

Kitaalamu, Bipolar imegawanyika katika aina kuu tatu zinazojumuisha Bipolar I yenye vipindi vikali vya mlipuko wa hisia vinavyoweza kumfanya mgonjwa  kuhitaji kulazwa hospitali, Bipolar II inayohusisha huzuni kali ya hali ya chini, pamoja na Cyclothymic Disorder ambayo ni mabadiliko ya hisia ya muda mrefu lakini yasiyo makali sana.

Ingawa ugonjwa huu hauna tiba ya kuuondoa kabisa, unaweza kudhibitiwa kwa kutumia dawa za kusawazisha hisia, dawa za kupunguza huzuni pamoja na tiba ya mazungumzo inayomsaidia mgonjwa kuelewa hali yake na kudhibiti hisia.

 Aidha, mtindo bora wa maisha kama kulala kwa wakati, kula lishe bora na kuepuka pombe pamoja na dawa za kulevya huchangia katika udhibiti wa dalili.

Wataalamu wanasisitiza kuwa watu wenye Bipolar wanaweza kuishi maisha ya kawaida na yenye tija iwapo watapata matibabu sahihi pamoja na msaada kutoka kwa jamii.

 Tanzania ina huduma za afya ya akili kuanzia ngazi ya vituo vya afya hadi hospitali, hivyo wananchi wanahimizwa kuwahi kutafuta msaada wa kitaalamu pindi wanapoona dalili kwao au kwa ndugu na marafiki.

Elimu na uelewa wa jamii ni nguzo muhimu katika kupunguza unyanyapaa na kuboresha maisha ya watu wanaoishi na ugonjwa wa Bipolar.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *