
Dar es Salaam. Baadhi ya waliokuwa wagombea urais katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025 kutoka vyama 16 vya siasa nchini, wamesisitiza umuhimu wa ajenda ya maridhiano kwa mustakabali wa Taifa, wakieleza kuwa kauli za kuwaita wenzao ‘wasaliti’ zinachangia kudhoofisha juhudi za kufikia muafaka wa kisiasa.
Wagombea hao walikutana na kufanya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan jana Jumatano, Aprili Mosi, 2026, ambapo walijadili hali ya kisiasa na masuala ya maendeleo ya Taifa.
Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya siasa waliotoa maoni yao kwa Mwananchi wameonyesha mitazamo tofauti kuhusu mwelekeo wa mazungumzo hayo, wakieleza kuwa licha ya hatua hiyo kuwa chanya, bado kuna haja ya kuwafikia wadau wote ili kufanikisha maridhiano ya kweli.
Taarifa ya mkutano huo ilitolewa na jana Aprili Mosi mwaka huu na kutiwa saini na Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Shaaban Kissu. Ikieleza kuwa Rais Samia alikutana na wagombea hao kufuatia ombi lao la kufanya majadiliano kuhusu hali ya kisiasa na maendeleo ya Taifa.
Katika kikao hicho, wagombea hao waliwasilisha maoni yao kuhusu namna ya kuimarisha maridhiano ya kisiasa, demokrasia ya vyama vingi, pamoja na kudumisha amani na mshikamano wa kitaifa baada ya uchaguzi mkuu huo.
Hatua hiyo inaendeleza ahadi ya Rais Samia aliyotoa Novemba 14, 2025 wakati wa uzinduzi wa Bunge la 13 jijini Dodoma, ambako alisisitiza kuendeleza juhudi za maridhiano nchini.
Katika hotuba hiyo, Rais Samia alisema ataendelea kunyoosha mkono wa maridhiano, akionesha matumaini kuwa wadau wa kisiasa wataupokea kwa dhati kupitia mifumo ya mazungumzo na usuluhishi ili kujenga mazingira ya muafaka kwa maendeleo ya Taifa.
Aidha, alirejea falsafa yake ya 4R inayojumuisha maridhiano (Reconciliation), mabadiliko (Reforms), ustahimilivu (Resilience) na kujenga upya (Rebuilding), akibainisha kuwa ndiyo msingi wa kuimarisha amani, utulivu na maendeleo endelevu nchini.
Sauti za wagombea
Aliyekuwa mgombea kupitia Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Yustas Rwamugira akizungumza na Mwananchi kwa simu leo Alhamisi Aprili 2, 2026, amesema maridhiano ni muhimu kwa Taifa, lakini akakosoa wanaowaita wenzao wasaliti.
Rwamugira amesema ushiriki wao katika uchaguzi mkuu ulikuwa ni utekelezaji wa matakwa ya kikatiba, hivyo haikuwa rahisi kujitoa katika mchakato huo.
“Yule ambaye haamini ushiriki wetu kwenye uchaguzi ndiye msaliti. Tuna Katiba inayoelekeza kufanyika kwa uchaguzi mkuu kila baada ya miaka mitano ili kupata kiongozi mwingine wa nchi,” amesema.
Kwa upande wake, mgombea mwenza wa urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Husna Abdalla Mohammed amesema maridhiano yana sura mbili kuu ambazo ni pamoja na ushiriki wa wananchi na vyama vya siasa.
Amesema katika kikao hicho walipata nafasi ya kuwasilisha maoni yao kuhusu namna ya kujenga Tanzania yenye amani na mshikamano baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.
“Tumetoa maoni kuhusu maridhiano na masuala ya maendeleo. Tukiona yanatekelezwa, tutakuwa na matumaini makubwa ya nchi kutulia na kurejea katika utulivu wa kweli,” amesema.
Akizungumzia madai kuwa wanatumika, amesema hiyo ni mitazamo ya baadhi ya wananchi, huenda ikichangiwa na matarajio ya waliodhani CUF isingeshiriki uchaguzi huo.
Naye aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Makini, Coaster Kibonde amesema uwepo wa vyama vingi nchini haupaswi kutafsiriwa kama uwanja wa kupinga kila jambo, bali ni fursa ya kufikia makubaliano kupitia majadiliano.
“Suala la maridhiano ni jema. Tunahitaji kuondoa sintofahamu na kuiweka nchi katika mazingira ya amani,” amesema.
Ameongeza kuwa kubezwa kwao ni jambo la kawaida kutokana na tofauti za mitazamo, huku akisisitiza kuwa walishiriki uchaguzi kwa kuzingatia sheria na Katiba.
Kwa upande wake aliyekuwa mgombea urais kupitia chama cha Sauti ya Umma (SAU), Majalio Kyara amesema mafanikio ya maridhiano yatategemea kuweka mbele maslahi ya Taifa.
Amesema ni muhimu kuanza mapema mchakato wa Katiba mpya ili kuepusha kujirudia kwa changamoto zilizojitokeza awali.
“Kususia michakato ya kitaifa hakusaidii kupata suluhu. Tunapaswa kushiriki ili kujenga mwafaka,” amesema.
Mitazamo ya wachambuzi
Ingawa Katiba ya Tanzania haitaji moja kwa moja maridhiano ya kisiasa, Ibara ya 9 inaweka msingi wa uongozi unaozingatia amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, mambo yanayotajwa kuwa nguzo za maridhiano.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Paul Loisulie amesema maridhiano ni muhimu akibainisha kuwa historia inaonyesha suluhu ya migogoro hupatikana kupitia mazungumzo.
Amesema uchaguzi uliopita uliibua mgawanyiko kutokana na misimamo tofauti kuhusu ushiriki wa vyama.
“Walioshiriki walionekana upande mmoja na waliokataa walibaki upande wao. Hali hiyo imezalisha tuhuma zinazoendelea hadi sasa,” amesema.
Ameongeza kuwa maridhiano yanapaswa kuwahusisha wadau wote, wakiwemo ambao hawakushiriki uchaguzi.
“Lipo kundi kubwa la Watanzania ambao hawakushiriki. Hawawezi kupuuzwa katika mchakato wa maridhiano,” amesema.
Mchambuzi mwingine, Magabilo Masambu amesema kukutana kwa Rais na wagombea hao ni hatua muhimu ya kupunguza mvutano wa kisiasa na kurejesha imani miongoni mwa wanasiasa.
Amesema hatua hiyo inaweza kusaidia kujenga upya mazingira ya ushindani wa kisiasa unaozingatia ushirikiano na demokrasia.
Kwa ujumla, mjadala wa maridhiano unaendelea kuchukua nafasi katika siasa za Tanzania, huku wadau wakitofautiana mitazamo kuhusu namna bora ya kuufanikisha, lakini wakikubaliana juu ya umuhimu wake kwa mustakabali wa Taifa.