Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limeimarisha doria katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, ikiwemo barabarani, visiwani na katika maeneo ya mikusanyiko ya watu, ili kuhakikisha wananchi wanasherehekea sikukuu ya Pasaka kwa utulivu na usalama.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema hatua hiyo inalenga kudhibiti vitendo vya uhalifu pamoja na ajali za barabarani zinazoweza kujitokeza wakati wa sikukuu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Aprili 3, 2026 katika ofisi yake, amesema jeshi hilo limeweka mikakati mbalimbali ya kuimarisha ulinzi ikiwemo kuongeza doria za magari, pikipiki, askari wa kiraia, askari wanaotumia wanyama pamoja na doria za boti katika maeneo ya visiwa vya Ziwa Victoria.

“Tumepanga askari katika maeneo yote muhimu ya mkoa. Kuna doria za magari kwenye makutano ya barabara, doria za pikipiki, doria za magari ya wazi, askari wa kiraia pamoja na askari wanaotumia wanyama. Pia tumeweka mpango wa doria za boti katika visiwa vilivyopo katika mkoa wetu,” amesema Mutafungwa.

Amesema pia ulinzi umeimarishwa katika barabara kuu zinazoingia na kutoka mkoani Mwanza kupitia magari maalumu ya ‘Highway Traffic Patrol’ kwa lengo la kudhibiti makosa ya barabarani yanayoweza kusababisha ajali.

Kamanda huyo amewataka wananchi wanaotarajia kusafiri au kusherehekea sikukuu nje ya makazi yao kuchukua tahadhari za kiusalama kwa kuhakikisha nyumba zao zinalindwa na kufungwa vizuri kabla ya kuondoka.

“Ni vyema familia zikahakikisha kuna mtu anabaki nyumbani kuangalia usalama wa mali zao. Usalama unaanza na wananchi wenyewe kabla ya jeshi la polisi,” amesema.

Aidha aliwataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto hawasherehekei sikukuu bila uangalizi wa watu wazima ili kuepusha matukio ya kupotea au kukumbana na hatari nyingine.

“Wakati mwingine baada ya sikukuu tunaanza kusikia taarifa za watoto kupotea, jambo ambalo mara nyingi hutokana na uzembe wa wazazi au walezi. Ni muhimu watoto wakawa chini ya uangalizi wa watu wazima,” amesema.

Pia amewataka wamiliki wa nyumba za kulala wageni na maeneo ya starehe kuzingatia masharti ya leseni zao pamoja na kuhakikisha usalama katika maeneo yao, huku akisisitiza kuwa ni marufuku kuendesha burudani za watoto maarufu kama ‘disko toto’ katika maeneo yasiyoruhusiwa.

Kwa upande wa madereva, Kamanda Mutafungwa aliwaonya dhidi ya kuendesha magari wakiwa wamelewa au kwa mwendo kasi, akisema askari watakuwa barabarani muda wote na hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa watakaokiuka sheria.

“Dereva yeyote atakayebainika kuendesha gari akiwa amelewa au kwa mwendo hatarishi atachukuliwa hatua mara moja bila kujali kuwa ni kipindi cha sikukuu,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *