
KUELEKEA mchezo kubwa wa Ligi Kuu Bara kati ya Azam dhidi ya Simba ‘Mzizima Dabi’, Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, ameweka wazi kuwa kikosi chake kipo tayari kwa mtihani huo mzito huku akiahidi maboresho yatakayowaongezea makali Wekundu hao wa Msimbazi.
Barker ambaye aliiongoza Simba juzi, Alhamisi kuifumua Coastal Union ya Tanga kwa mabao 2-0 na kuifanya timu hiyo kufikisha pointi 34 katika nafasi ya pili, amesema mchezo wa Jumapili ambao utapigwa kwenye Uwanja wa Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam ni moja ya mechi kubwa wanazozisubiri kwa hamu, akieleza kuwa ndiyo aina ya michezo inayopima kiwango halisi cha timu. “Hizi ndizo mechi tunazotaka kucheza. Utakuwa mtihani mzuri wa kuona tupo wapi na tunataka kufika wapi,” amesema akiongea na Mwanaspoti.
Kocha huyo ameongeza kuwa licha ya Simba kuonyesha kiwango kizuri katika michezo ya hivi karibuni, bado kuna maeneo muhimu wanapaswa kuyaboresha, hususani umakini wa kutumia nafasi wanazotengeneza na kulinda mpira wanapokuwa nao katika eneo la mwisho.
Kocha huyo raia wa Afrika Kusini, amesisitiza kuwa endapo watakuwa makini zaidi katika eneo la ushambuliaji na umiliki wa mpira, basi watakuwa tishio kubwa zaidi kwa Azam inayonolewa na Mkongomani, Florent Ibenge.
“Ni muhimu kuwa makini zaidi mbele ya lango. Tunatengeneza nafasi nyingi, lakini tunahitaji kuzitumia vizuri zaidi,” amesema.
Aidha, Barker ameeleza kuwa kikosi chake kitapata nguvu zaidi kuelekea mchezo huo baada ya baadhi ya wachezaji waliokosekana katika mchezo uliopita kurejea akiwemo beki wake mahiri, Rushine De Reuck na Yusuph Kagoma (walipumzishwa) huku akibainisha kuwa mzunguko wa wachezaji ni muhimu kutokana na ratiba ngumu ya mechi zilizosalia.
“Tuna mechi nyingi zilizobaki, hivyo ni muhimu kila mchezaji apate nafasi na wengine wapate muda wa kupumzika,” amesema.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, Simba ilikiona chamoto mbele ya Azam kwa kuchapwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa hivyo hii itakuwa ni mechi ya kisasi kwa Mnyama huku Azam ambayo ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo ikiwa na pointi 32 ikihitaji kuendeleza ubabe wake.
Wababe hawa wanakutana huku wakiwa na rekodi zinazokaribiana, Simba katika mechi 15 imefunga mabao 26, ikiwa na wastani wa mabao 1.73 kwa kila mechi, huku ikiruhusu mabao sita pekee. Kwa upande wa Azam FC, wao wamecheza mechi 16 wakifunga mabao 23, wastani wa mabao 1.44 kwa kila mechi, huku wakiruhusu mabao matano.