
UONGOZI wa KMC FC umefikia makubaliano ya kuachana na Abdallah Mohamed ‘Baresi’, kwa maku-baliano ya amani ya pande zote mbili, huku kocha huyo akidumu kwa siku 94, sawa na miezi mitatu na siku nne, akiondoka na kuacha rekodi mbovu kikosini.
Uamuzi wa kuachana na Baresi, ulifikiwa juzi Aprili 3, 2026, ikiwa ni muda mfupi tu tangu kocha huyo achapwe mabao 3-2, dhidi ya Mbeya City, katika mechi ya Ligi Kuu iliyopigwa kwenye Uwanja wa Tan-zanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara.
Baresi aliyejiunga na KMC FC, Desemba 30, 2025, akichukua nafasi ya Mbrazil Marcio Maximo ali-yeondoka, Desemba 6, 2025 amekiongoza kikosi hicho katika mechi nane za Ligi Kuu msimu huu, am-bapo ameshinda moja, sare moja na kupoteza sita.
Mechi aliyoshinda kocha huyo ni ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mashujaa FC, Februari 3, 2026, ingawa, baada ya hapo amekuwa na mwenendo usioridhisha, huku kati ya hiyo nane aliyoiongoza alifunga mabao matano na kuruhusuru 14.
Kwa msimu wa 2025-2026, Maximo aliiongoza KMC katika jumla ya mechi tisa za Ligi Kuu, ambapo kati ya hizo alishinda moja tu, sare moja na kuchapwa saba, huku kikosi hicho kikifunga mabao mawili na kuruhusu 14, akikiacha mkiani na pointi nne.
KMC inayoburuza mkia na pointi nane, imecheza mechi 17 za Ligi Kuu Bara, ambapo imeshinda mbili, ikitoka pia sare mbili na kupoteza 13, huku safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho ikifunga mabao saba na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 28.
Akizungumza baada ya kuachana na timu hiyo, Baresi alisema ameamua kufanya uamuzi wa busara na kuachia wengine kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa kikosi hicho, licha ya matarajio pia ma-kubwa aliyopewa na uongozi wakati anajiunga nayo.
“Kwa nilipofikia na mwenendo wetu kiukweli nimeamua niachie nafasi wengine ili waendeleze nili-poishia, malengo yalikuwa kufanya vizuri lakini, inapotokea tofauti na matarajio niliyojiwekea, kama kocha ni lazima niwajibike,” alisema.
Baresi aliyewahi kuzifundisha timu mbalimbali zikiwemo za maafande wa JKT Tanzania, Tanzania Pris-ons na Mashujaa FC za Bara, alijiunga na KMC FC, baada ya kuachana na Zimamoto ya visiwani Zanzibar, huku akiwahi pia kuifundisha Mlandege FC.