
Dar es Salaam. Sakata la kupanda kwa bei ya mafuta linazidi kuchukua sura mpya, baada ya Umoja wa Wasafirishaji Tanzania (TAT) kuitahadharisha Serikali kuchukua hatua za haraka kupunguza ushuru na tozo, la sivyo uchumi wa nchi utatikisika.
Wasafirishaji hao wa barabara, maji na reli wamesema mapato ya Serikali yatapungua, matumizi ya Reli ya Kisasa (SGR) na bandari yatayumba kwani mataifa mbalimbali yanayozitumia yatatafuta maeneo mengine ili kuhimili gharama za mafuta.
Umoja huo wa wasafirishaji umetoa kilio hicho kwa Serikali ikiwa ni siku ya tatu tangu Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) ilipotangaza Aprili 1, 2026 ongezeko hilo la bei za mafuta, linaloelezwa kuchochewa na mgogoro wa kimataifa unaoendelea kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran ulioanza Februari 28, 2026.
Mgogoro huo umeathiri uzalishaji na usafirishaji wa mafuta ghafi duniani, hasa baada ya kufungwa kwa Mlango wa Hormuz, ambao hupitisha takriban asilimia 20 ya mafuta yote yanayosafirishwa duniani.
Vilevile, kushambuliwa kwa visima vya mafuta, maghala ya kuhifadhi mafuta na viwanda vya kuyasafisha kumeigusa moja kwa moja Tanzania, ambayo inaagiza mafuta kwa kiasi kikubwa, jambo linalotajwa kuongeza gharama za usafirishaji kutokana na kukosekana kwa meli za kuyasafirisha.
Hali hiyo imesababisha ongezeko kubwa ambalo halijashuhudiwa kwa zaidi ya miaka 20, na kuilazimisha Serikali kukaza mikakati ya kupunguza athari hizo, kama alivyoeleza Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, bungeni jijini Dodoma.
Aprili Mosi, 2026, akiwasilisha makadirio ya bajeti ya ofisi yake kwa mwaka 2026/27 ya Sh12.5 trilioni, Dk Mwigulu amesema:
“Tumeona bei zimeshaanza kupanda, tutakaa ndani ya Serikali kuhakikisha tunakabiliana nalo vipi suala hili ili wananchi waendelee kupata mafuta kwa bei nzuri na kudhibiti kupanda kwa gharama za maisha.”
Hata hivyo, Dk Mwigulu alisema licha ya changamoto zinazoendelea Mashariki ya Kati, amewahakikishia Watanzania Serikali itaendelea kusimamia upatikanaji wa petroli na dizeli ili kuhakikisha zinaendelea kuwa himilivu.
Licha ya maelezo hayo ya Serikali, wadau mbalimbali wameendelea kupaza sauti wakiomba nafuu ya kupunguzwa kwa ushuru na/au tozo za bidhaa hizo ili kupunguza maumivu kwa wananchi.
Baadhi ya shughuli zimeanza kuathirika kwa ongezeko hilo la mafuta la zaidi ya Sh900 kwa lita, ikiwemo nauli za usafiri kama daladala, bajaji na bodaboda, huku wale wa mabasi ya mikoani nao wakilalama gharama kubwa za uendeshaji.
Tayari Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra), Habibu Suluo, ametangaza kuitisha kikao cha wadau wa usafirishaji Aprili 8, 2026 jijini Dar es Salaam, ambacho kitajadili suala hilo na kutoa uamuzi.
Ilichosema TAT
Katikati ya mijadala hiyo, Umoja wa Wasafirishaji Tanzania (TAT) umeiandikia barua Ewura wakionyesha mzigo wanaoupata na kuomba hatua za haraka zichukuliwe kama mataifa ya Namibia, Zambia na Afrika Kusini kupunguza ushuru na tozo.
Katika barua hiyo kwenda Ewura yenye kurasa tatu ya Aprili 2, 2026, iliyosainiwa na Rais wa TAT, Omar Kiponza, inaeleza bei ya juu ya mafuta itasababisha uharibifu wa mahitaji ambapo idadi ya magari barabarani inapungua, hivyo kupunguza jumla ya kodi inayokusanywa kutokana na mauzo ya mafuta.
Amesema mafuta yanachangia takribani asilimia 40 hadi 55 ya gharama za uendeshaji kwa wanachama wao wa barabara na majini, hivyo ongezeko hilo litafanya mikataba ya muda mrefu ya usafirishaji kutokuwa na tija kiuchumi.
Kwa mujibu wa sekta ya usafirishaji, amedai ni mchangiaji wa pili kwa ukubwa wa fedha za kigeni baada ya utalii, ambapo kwa mwaka 2025 ilichangia zaidi ya dola bilioni 2.7 sawa na Sh2.75 trilioni.
“Kupanda kwa bei ya mafuta, ukiacha athari za kupungua kwa mapato, pia ni tishio kwa uwekezaji wa bandari kwani linahatarisha ufanisi wa bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara.
Gharama kubwa za usafirishaji wa nchi kavu zitawafanya majirani Zambia, DRC, Rwanda na Malawi kutafuta korido mbadala kama Beira (Msumbiji) au Walvis Bay (Namibia),” amesema Kiponza.
Kwa upande wa usafiri wa reli ya kisasa (SGR) iliyoanza huduma ya makontena Februari 2026, amesema iko hatarini kukwama kwa sababu usafirishaji wa kilometa ya mwisho unategemea malori yanayotumia mafuta ya bei ghali.
“Kwa namna hii, bila hatua za haraka, miundombinu yetu ya kisasa ya bandari na reli inaweza kubaki bila kutumika kwa sababu gharama ya kutoa mizigo bandarini kuelekea mipakani itakuwa kubwa mno.
Hivyo, tunasubiri hatua za haraka ili kulinda uchumi wa kila siku wa Watanzania na kuokoa sekta ya usafirishaji,” amesema Kiponza.
Leo Jumamosi, Aprili 4, 2026, Mwananchi limemtafuta Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, kuhusu barua hiyo ya TAT na hatua ambazo Serikali inazichukua, amesema:
“Serikali inafanyia kazi jambo hili kwa umuhimu mkubwa,” amesema Msigwa.
Wataalamu wanachakata namna bora ya kufanya na wakati wowote Serikali itatoa mwelekeo tutakaochukua. Tunawaomba wananchi wavumilie, muda mfupi ujao watajulishwa,” amesema Msigwa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Mwananchi limemtafuta Msigwa kwani Aprili 2, 2026, Rais Samia alitangaza kutengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Dk. James Mwainyekule na kueleza atapangiwa kazi nyingine. Taarifa ya utenguzi haikueleza nani atakaimu au atashika nafasi yake.
Shakua, abiria
Mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Abiria (Shakua), Hashim Omar amesema kihalisia mafuta yakipanda, hali ya uchumi pia hupanda.
Hata hivyo, Latra ikikataza wamiliki wa daladala kupandisha nauli, huko mtaani tayari limeanza kufanyika, na mamlaka imeitakiwa kwenda mtaani kuchukua hatua ili iwe fundisho kwa wengine.
Kuhusu bajaji na bodaboda kupandisha bei zaidi ya mara mbili, Omar amesema asingependa kuzungumzia, kwa kuwa usafiri huo upo kwa ajili ya kukodiwa na siyo kama daladala; hivyo ni uamuzi wa abiria kupanda au kuacha.
Mmoja wa abiria aliyejitambulisha kwa jina la Husna amesema usafiri wa bodaboda na bajaji umekuwa mkombozi kwa wananchi wengi, ukirahisisha usafiri kutoka eneo moja kwenda jingine na kuondoa usumbufu wa kukaa muda mrefu barabarani.
Abdallah Juma, mkazi wa Mbezi jijini Dar es Salaam, amesema gharama za bajaji kutoka Mbezi hadi Mwenge zimepanda; ambapo awali ilikuwa Sh2,000, sasa imefikia kati ya Sh2,500 hadi Sh3,000 kwa kila mmoja.
Sakina Hegga anasema awali alikuwa akipanda bajaji kutoka Kinyerezi hadi Mbezi kwa Sh1,000, sasa imefikia Sh1,500, na kutoka Malamba hadi Mbezi ilikuwa Sh500, sasa imefikia Sh1,000. Kuongezeka kwa nauli hizi huongeza muda wa safari asubuhi au jioni.
Joel Meshack, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Nyama Machinjio ya Vingunguti, amesema ongezeko la bei ya mafuta limewaathiri kwani gharama za usafirishaji wa mifugo na nyama zimeongezeka pia.
Meshack ametolea mfano gari walilokuwa wakikodi kusafirisha mifugo kutoka Dodoma kuja Dar es Salaam, walilipa Sh1 milioni, sasa gharama imeongezeka hadi kufikia Sh1.3 hadi 1.5 milioni.
“Kama hali itaendelea kuwa hivi, pengine bei ya nyama inaweza kuongezeka; kwa sasa inauzwa kati ya Sh11,000 hadi 12,000 kwa kilo,” amesema Meshack.