MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) kupitia Idara ya upelelezi wa kodi kanda ya nyanda za juu kusini, Imewafikisha mahakamani Watu wawili kwa tuhuma za kukiuka sheria za ushuru wa bidhaa na kufanya uzalishaji wa pombe kali bila kibali halali.
Meneja wa TRA Mkoa wa Ruvuma, Bwana Nicodemus Mwakilembe, amewataja washtakiwa hao kuwa ni Khadija Hiza na Abraham Mosile ambao wanadaiwa kubandika stika za ushuru wa bidhaa na kuzalisha pombe bila kuwa na leseni kutoka kwa Kamishna wa Kodi za ndani kinyume na taratibu za Sheria za Kodi nchini.
Wakili wa Serikali Mwandamizi kutoka TRA, Medalakini Emmanuel, amesema kesi hiyo imesomwa katika Mahakama ya wilaya ya Songea chini ya hakimu mkazi mwandamizi Christina Haule ambapo watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na bidhaa za pombe kali aina ya La Chalz Beverages Lion Spirit, ambazo zilipaswa kulipiwa ushuru wa bidhaa lakini zilikutwa zikiwa na stempu za kielektroniki bandia.
Wakili Emmanuel amesema kuwa kati ya makosa nane yanayowakabili watuhumiwa hao, matatu ni ya kukutwa na bidhaa zilizopaswa kulipiwa ushuru wa bidhaa zikiwa na stempu bandia, huku makosa mengine yakihusisha kukwepa kodi kwa udanganyifu wa kubandika stempu zisizo halali.
Aidha, kosa la nane ni la uhujumu uchumi, ambapo watuhumiwa wanadaiwa kuisababishia TRA hasara kutokana na kitendo cha kukwepa kulipa kodi stahiki.
(Feed generated with FetchRSS)