Dar es Salaam. Katika jitihada za kulinda afya ya umma na kuinua viwango vya usalama wa chakula, sekta ya hoteli nchini imeendelea kuchukua hatua kuhakikisha huduma zinazotolewa zinazingatia viwango vinavyotambulika kimataifa.

Hyatt Regency Dar es Salaam, The Kilimanjaro imepokea tena cheti cha usalama wa chakula cha HACCP (Hazard Analysis and Critical Control Points), kinachotolewa kwa ushirikiano na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) pamoja na mamlaka nyingine za udhibiti wa ubora wa chakula. 

Hatua hiyo inaonyesha dhamira endelevu ya hoteli hiyo katika kuzingatia viwango madhubuti vya usimamizi wa usalama wa chakula. Mwaka 2023, hoteli hiyo ilikuwa ya kwanza jijini Dar es Salaam kupata cheti hicho, hivyo kuweka kigezo cha ubora katika sekta ya usimamizi na udhibiti ubora wa vyakula.

Cheti hicho hutolewa kwa kuzingatia maeneo yote muhimu ya mnyororo wa chakula ndani ya hoteli hiyo, yakiwemo mapokezi na uhifadhi wa malighafi, uandaaji wa chakula, huduma za upishi pamoja na utoaji wa chakula kwa wateja. Maeneo hayo yako chini ya kundi la huduma za chakula (Food Category Code E), linalojumuisha huduma za chakula kwa ujumla.

Uendelevu wa cheti hicho utategemea ukaguzi wa mara kwa mara unaofanywa na TBS, ili kuhakikisha viwango vilivyowekwa vinaendelea kufuatwa ipasavyo.

Akizungumza hatua hiyo jijini Dar es Salaam, Dk Ashura Katunzi, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, amesema cheti hicho kinaonyesha umuhimu wa kuzingatia mifumo ya usalama wa chakula katika kulinda afya ya watumiaji na kuimarisha imani kwa sekta ya ukarimu.

“Hoteli na watoa huduma za chakula wanapaswa kuzingatia viwango vya kimataifa ili kulinda afya ya umma. Hii inaonyesha kuwa taasisi husika imekidhi vigezo na inaendelea kufuata kanuni za kitaifa na kimataifa,” amesema.

Kwa upande wake, Alexander Eversberg, Meneja Mkuu wa hoteli hiyo, amesema kuendelea kuwa na cheti hicho ni uthibitisho wa dhamira ya kutoa huduma bora.

“Tunajivunia kuendelea kuwa na cheti cha HACCP, kinachothibitisha dhamira yetu ya kutoa chakula salama na huduma bora kwa wageni wetu. Tunaendelea kuboresha utendaji wetu ili kukidhi na kuzidi matarajio,” amesema.

Naye Gabriellah Temba, Meneja wa Usalama wa Chakula na Usafi (Hygiene Manager) wa hoteli hiyo, amesema cheti hicho kitasaidia kuvutia wateja zaidi na kuimarisha imani yao kitaifa na kimataifa.

“Cheti hiki kwetu ni zaidi ya biashara; ni alama ya kuaminika na uhakika wa usalama kwa kila anayechagua huduma zetu,” amesema.

Kwa kuendana na matakwa ya kitaifa na mbinu bora za kimataifa, hoteli hiyo imeendelea kujijengea taswira ya kuaminika kwa wateja wa ndani na nje ya nchi, wakiwemo wafanyabiashara, viongozi wa Serikali na wageni wa kidiplomasia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *