
Mauaji hayo yalitokea Machi 24 katika eneo la uchimbaji madini la Karhembo mashariki mwa DRC, ambapo mashirika ya kiraia ya eneo hilo yanalaani kuanzishwa kwa hali ya ugaidi. Kulingana na mashahidi kadhaa, wachimbaji hao walipigwa risasi na kuuawa wakati wakidai kulipwa angalau miezi mitano ya mishahara ya nyuma.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kulingana na takwimu rasmi, angalau wachimbaji madini 13 wa Kongo waliuawa na wapiganaji wa AFC/M23, Machi 24, katika eneo la uchimbaji madini la Karhembo katika mkoa wa Kivu Kusini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Katika taarifa, jeshi la Kongo pia lilishutumu kundi hilo lenye silaha kwa kutekeleza mauaji hayo, ambayo baadhi ya wafuasi wake walijibu kwa kushutumu madai haya kuwa “hayana msingi na hayajathibitishwa.”
“Uvumi ulisambaa kwamba kulikuwa na watu kama zaidi ya hamsini waliofariki lakini tumethibitisha 13 pekee,” mkazi wa Walungu ameiambia RFI, akiongeza kuwa anasikitishwa kwamba baadhi ya wachimbaji walichukuliwa kimakosa kuwa ni wapiganaji wa Wazalendo, wanamgambo wanaopigana katika safu ya jeshi la serikali, FARDC. “Walikuwa wakifanya kazi kwa niaba ya AFC/M23, ambayo inadhibiti eneo hilo kwa karibu mwaka mmoja na inachimba dhahabu kinyume cha sheria huko,” chanzo hicho kimeongeza.
Kwa upande wake,shirika linalojihusisha masuala ya usalama katika mikoa ya Kivu linaripoti idadi ya “watu 40 ambao waliuawa na 14 waliojeruhiwa.”
Hali ya ugaidi
Wachimbaji madini hao walipigwa risasi na kufa huku wakidai kulipwa angalau miezi mitano ya mishahara ya nyuma, mashahidi kadhaa wameiambia RFI, wakibainisha kuwa wapiganaji wa AFC/M23 waliwapiga risasi baada ya kuwashutumu kwa kujaribu kuvuruga usalama wa eneo hilo.
Kufuatia mauaji hayo, mashirika ya kiraia katika eneo hilo yamelaani hali ya ugaidi inayotawala katika kijiji cha madini cha Karhembo na mazingira yake, ikiripoti kwamba, wanakabiliwa na hali hii, wachimbaji madini hawarudi tena kwenye eneo hilo na wengine wamechagua hata kuondoka vijijini mwao. “Ni wapiganaji wa AFC/M23 pekee waliokusanyika huko, wakiandamana na washirika wachache wa kiraia,” amesema mmoja wa watu hawa, ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Kulingana na Didier Kabi, msemaji wa serikali ya mkoa wa Kivu Kusini, mamlaka ya Kongo inafuatilia kwa karibu hali hiyo.