Nigeria. Ni miaka 12 imepita tangu mwimbaji kutokea Nigeria, Yemi Alade, 37, afanye vizuri na wimbo wake, Johnny (2013) ambao ulikuja kujumuishwa katika albamu yake ya kwanza, King of Queens (2014) chini ya Effyzzie Music Group.

Hata hivyo, hadi sasa bado Yemi Alade ‘anamsaka mwanaume’ aliyemwimba katika wimbo huo (Johnny) uliopata mafanikio makubwa katika nchi za Nigeria, Tanzania, Kenya, Zambia, Ghana, Afrika Kusini, Liberia, Uganda na Zimbabwe.

“Ninamtafuta Johnny wangu, yuko wapi Johnny wangu?. Unamjua Johnny? nauliza. Kama nisipompata Johnny wangu nitaumia sana,” anaimba Yemi Alade katika wimbo huo uliotayarishwa na Selebobo.

Yemi Alade katika wimbo huo anaibainisha kuwa Johnny amemkimbia na kwenda kwa Cynthia kwa madai ndiye anamridhisha. Wakati huo huo amempa mimba Uche lakini anataka kumuoa rafiki yake Nene, kitu ambacho kinamtesa.

Wimbo huo ambao kabla ya kutolewa rasmi uliwahi kuvuja mtandaoni, uliendelea kufanya vizuri kwa miaka mingi na ilipofika Agosti 2025, Jarida la Billboard liliuweka nafasi ya 15 kwenye orodha ya nyimbo 50 bora za Afrobeats za muda wote.

Video ya wimbo huo iliachiwa Machi 3, 2014, ikizinduliwa kupitia Vevo na YouTube huku ikiwa imeongozwa na Clarence Peters. Video inaanza kwa kumuonyesha mchekeshaji Bovi ambaye anajitokeza kama mtangazaji wa kipindi kinachofichua wapenzi wasio waaminifu.

Kufikia Januari 2019, video hiyo ikaweka rekodi ya kutazamwa mara milioni 100 katika mtandao wa YouTube, na kumfanya Yemi Alade kuwa msanii wa kwanza kike Afrika kufikia mafanikio hayo, na wa pili Nigeria baada ya Davido.

Hata hivyo, hadi sasa Yemi Alade ameshindwa kuwa na video nyingine yenye namba kama hizo licha ya kutoa kazi nyingi lakini bado anaendelea kuisaka rekodi ya Johnny. Na ndio sababu tunasema bado anamsaka Johnny wake!.

Video ya Johnny ambayo hadi sasa imetazamwa mara milioni 181 YouTube, inafuatiwa na ya wimbo, Bum Bum (2018) iliyotazamwa mara milioni 55 ikiwa haijafikia hata nusu ya Johnny, hivyo ni wazi Yemi Alade bado ana kazi kubwa ya kumtafuta Johnny.

Machi 2024, Yemi Alade aliadhimisha miaka 10 ya Johnny (2014), kupitia Instagram akisema tangu kuachiwa kwa kazi hiyo maisha yake yalibadilika kwenye kila kitu, jambo ambalo anashukuru hatua hiyo kubwa.

Ikumbukwe jina la Yemi Alade lilianza kuchomoza baada ya kushinda mashindano ya kusaka vipaji, Peak Talent Show 2009, na kisha kupata nafasi ya kusainiwa na Effyzzie Music Group kabla ya kutoka na wimbo wake huo, Johnny (2014).

Baada ya kutoa albamu zake mbili za mwanzo, alianza kufanya ziara za kimataifa, na baadaye akashinda tuzo za MTV MAMAs kama Msanii Bora wa Kike 2015 & 2016, jambo lililomfanya kuwa mwanamke wa kwanza kushinda tuzo hizo mara mbili mfululizo.

Mwaka huohuo 2015, alikuwa mwanamke wa kwanza kutoka Afrika kuteuliwa kuania tuzo za MTV EMAs, na pia aliteuliwa kwenye BET akiwania kipengele cha Msanii Bora wa Kimataifa Afrika 2015 & 2016.

Tayari Yemi Alade ametoa albamu sita ambazo ni King of Queens (2014), Mama Africa (2016), Black Magic (2017), Woman of Steel (2019), Empress (2020), na Rebel Queen (2024). Na pia ametoa Extended Playlist (EP) nne, Mama Afrique (2017), Queendoncom (2021), African Baddie (2022), na Mamapiano (2023).

Albamu yake ya mwisho, Rebel Queen (2024) ilitoa wimbo Tomorrow ambao uliteuliwa kuwania tuzo za 67 za Grammy 2025 katika kipengele cha Msanii Bora Afrika, ikiwa ni mara yake ya kwanza kupata nafasi hiyo.

Mafanikio mengine ya Yemi Alade ni kuwa miongoni mwa wasanii wa Afrika walioshirikishwa na mwimbaji wa Marekani, Beyonce Knowles katika albamu yake, The Lion King: The Gift (2019).

Katika albamu hiyo ya Beyonce, alisikika kwenye nyimbo mbili, Don’t Jealous Me na My Power. Mbali na Yemi Alade, wasanii wengine waliopata nafasi ni Burna Boy, Mr. Eazi, Tiwa Savage, Tekno, Wizkid na kadhalika.

Desemba 2024, Yemi Alade aliiambia CNN alipoteza sauti katika hali ya kushangaza sana baada ya kuwasili Los Angeles, Marekani ili kushirikiana na Beyonce, jambo ambalo alilihusisha na imani za kishirikina kutoka kijijini kwao.

Mara moja alifanya mpango wa kurejesha sauti yake akitumia mchanganyiko wa maji moto, vitamini C, tangawizi na chai, baada ya mafundo kadhaa sauti yake ilirejea na kuweza kurekodi nyimbo mbili na Beyonce, mshindi wa Gramm 35.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *