Zanzibar. Hivi unajua sheria inayosimamia dawa za kulevya inataka kuitwa mashahidi huru wawili wakati wa upekuzi? Hii ndio dosari ya kisheria ambayo imeifanya Mahakama ya Rufani Zanzibar kumwachia huru, Rashid Hamad Ali.

Kifungu 42(2) cha Sheria ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar (ZDCEA ), kinasema kamishna au ofisa aliyeidhinishwa, wakati wa upekuzi ataalika mashahidi wawili huru kushuhudia.

Hata hivyo, hilo halikufanyika Julai 11,2022 eneo la Pujini Dodo, Wilaya ya Mkoani huko Pemba wakati maofisa wa ZDCEA walipomkamata Ali, wakimtuhumu kupatikana na vipuli 101 vyenye unga wa dawa za kulevya aina ya heroin.

Hii ni sababu imewafanya majaji wa Mahakama ya Rufani Zanzibar, Barke Sahel, Issa Maige na Lameck Mlacha kuona upande wa mashitaka haukuwa umethibitisha shitaka hilo, hivyo kubatilisha kifungo cha miaka 30 na kumwachia huru Ali.

Hii ni baada ya kukata rufaa akipinga hukumu hiyo aliyopewa Desemba 12, 2022, akiegemea sababu sita za rufaa kwamba shitaka hilo halikuwa limethibitishwa na pia kulikuwa na kukatika kwa mnyororo wa utunzaji kielelezo wakati wa ukamataji.

Hukumu hiyo ya Mahakama ya Rufani ilitolewa Juni 19,2026 lakini ikapandishwa katika tovuti ya Tanzlii Juni 21,2026 ambayo ni tovuti ya Serikali ya Tanzania inayochapisha hukumu,uamuzi, sheria na kanuni bure mtandaoni.

Ushahidi wa Jamhuri ulivyokuwa

Kulingana na ushahidi wa shahidi wa pili ambaye ni Ofisa wa ZDCEA, Hassan Juma Hamad, alieleza kuwa Julai 11,2022 akiwa kazini, alipokea taarifa fiche kutoka kwa msiri wake, akimjulisha kuwa Ali anajihusisha na dawa za kulevya.

Katika kuifanyia kazi taarifa hiyo na akiwa ameambatana na shahidi namba 5 ambaye pia ni ofisa wa ZDCEA, walikwenda eneo la Pujini Dodo walikoelekezwa na ilipofika saa 11:40 alasiri, walidai kumuona Ali akitembea barabara kuu.

Walimsogelea, wakajitambulisha kuwa wao ni maofisa kutoka ZDCEA  na kumtaka atoe ushirikiano ili wampekue mwilini, ombi ambalo lilikubaliwa na Ali.

Kwa mujibu wa ushahidi, shahidi huyo alitoa kimfuko kidogo cha plastiki katika mfuko wa kulia wa suruali yake, ambacho kilikuwa na vipuli 101 vilivyokuwa na unga wa rangi ya kahawia ambavyo walivishuku vina dawa za kulevya.

Mara moja alikamatwa pamoja na kielelezo na kupelekwa ofisi za ZDCEA ambako kulifanyika uhesabuji na kubainika ni vipuli 101 na jalada lilifunguliwa na kielelezo kiliwekwa katika bahasha na kukabidhiwa kwa mtunza vielelezo.

Baadaye mtunza vielelezo huyo, Jape Khatib Haji ambaye alikuwa ni shahidi namba tatu wa upande wa mashitaka, alitoa kielelezo hicho na kumkabidhi shahidi namba 4, ambaye naye akamkabidhi shahidi namba moja, Mauwa Kombo Khamis.

Khamis ambaye ni mkemia wa Serikali, alifungua bahasha hiyo na kuhesabu vijifuko vilivyokuwepo na kuthibitisha ni 101 na katika uchunguzi wa kimaabara, alithibitisha unga uliokuwepo ndani yake ni heroin yenye uzito wa gramu 2.343.

Baadaye kielelezo hicho kilirudishwa kwa shahidi namba nne ambaye naye alimkabidhi shahidi namba tatu kwa ajili ya kuvitunza hadi kilipotolewa mahakamani kama kielelezo PE1 baada ya mshitakiwa kufikishwa mahakamani.

Alivyokana kukamatwa na heroin

Katika utetezi wake mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi, Chake Chake Pemba, mshitakiwa alikanusha tuhuma hizo na kueleza kuwa maofisa hao wa ZDCEA walimtuhumu kimakosa kuwa anajihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Alidai kuwa walimtisha kuwa wangemkamata na kumbambikia dawa hizo.

Aliendelea kudai kuwa siku za nyuma, maofisa wa ZDCEA waliwahi kumpekua lakini hawakumkuta na kitu chochote ambapo alidai taarifa kuwa ofisa wa ZDCEA alimpiga simu na kumjulisha kuwa amekamatwa na dawa ulikuwa ni uongo.

Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande mbili, hakimu mkazi aliyesikiliza kesi hiyo aliridhika kuwa upande wa mashitaka ulikuwa umethibitisha kosa hilo na iliwaamini zaidi shahidi namba mbili na tano ambao walifanya ukamataji huo.

Hakimu huyo alisema ushahidi wao ulikuwa umeungwa mkono na shahidi namba moja wa upande wa mashitaka ambaye ni mkemia wa Serikali ambaye alichunguza kielelezo alichopelekewa na kuthibitisha kuwa ilikuwa ni dawa za kulevya.

Jamhuri yamuunga mkono mshitakiwa

Mshitakiwa alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, lakini hakuridhika na kutiwa kwake hatiani na adhabu aliyopewa na ndipo alipokata rufaa kupinga hukumu.

Wakati wa usikilizwaji wa rufaa, mshitakiwa alisimama mwenyewe wakati Jamhuri ikiwakilishwa na wakili wa Serikali mkuu, Mohamed Ali Juma, aliyesaidiana na mawakili, Ali Juma Makame, Asya Ibrahim Mohamed na Zalha Makame Juma.

Wakili wa Serikali mkuu, Mohamed Ali Juma alikubaliana na hoja za mrufani kwamba mjibu rufaa ambaye ni Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP), hakuwa ameweza kuthibitisha shitaka pasipo kuacha mashaka kama sheria inavyotaka.

Alirejea ukurasa wa tisa na 18 wa hukumu iliyomfunga shahidi namba mbili na tano ambao walielezea kwa kirefu mazingira ya ukamataji wa mrufani ulivyofanyika.

Katika ushahidi wao, walieleza kuwa mrufani huyo alizuiwa, kupekuliwa na kukamatwa eneo la makazi lakini hakuna mashahidi wa huru waliohusika.

Wakili huyo aliendelea kueleza kuwa kulingana na aina ya ushahidi ulitolewa kortini, ni kwamba ukamataji huo ulifanyika mchana, maofisa wa ZDCEA walipaswa kutafuta mashuhuda huru wawili.

Kwa mujibu wa wakili huyo, kwa kuwa ushahidi uko kimta wa kama kulikuwa na sababu inayokubalika ya kushindwa kutafuta mashahuda huru,  basi hakuna sababu inayokubalika inayowapa uhalali shahidi namba mbili  na tano kutowatafuta.

Alieleza kuwa uwepo wa mashuhuda huru wawili ni wa lazima kisheria na kwamba uwepo wa shahidi huru ulikuwa ni kulinda uadilifu wa mchakato wa upekuzi.

Majaji walivyomwachia huru

Baada ya kusikiliza hoja za pande mbili, majaji wa Mahakama ya Rufani walisema kulikuwa hakuna ubishi kuwa wakati wa kumpekua mrufani kulikuwa hakuna mashahidi huru, licha ya barabara alipokamatwa kuwa na shughuli na watu wengi.

“Ilikubalika kuwa haikuwa upekuzi wa dharura. Bila shaka, isingekuwa dharura kwa sababu shahidi namba mbili na tano walielekea Pujin Dodo baada ya kupokea taarifa za kiintelijensia kuwa mrufani alikuwa anajihusisha na dawa za kulevya,” walisema.

Majaji hao walisema kama alivyoeleza wakili wa Serikali mkuu, mashuhuda huru ni kwa ajili ya kulinda haki za mshukiwa kwa kuzuia upekuzi holela na huongeza uaminifu na uwazi wa mchakato wa upekuzi kwa kutoa uthibitisho usio na upendeleo wa kile kilichotokea wakati wa ukaguzi na utafutaji.

Katika rufaa hiyo, walisema mrufani alipekuliwa katika eneo lenye shughuli nyingi na watu wengi likiwa limezungukwa na makazi ya watu na hiyo inaonyesha kulikuwa na mazingira mazuri kwa maofisa wa ZDCEA kupata mashuhuda huru.

“Kwa ushahidi wao wenyewe (shahidi namba mbili na tano) wanathibitisha kuwa upekuzi ulifanyika wakati wa mchana saa 11. Kwa mazingira hayo hatuoni uhalali wowote kwa maofisa hao kutozingatia kifungu namba 42(2 cha sheria ya ZDCEA,” walisema.

“Hii kushindwa kuita mashahidi huru kunadhoofisha uadilifu wa ushahidi wa shahidi namba mbili na tano na kielelezo kilichopatikana. Hatuna mashaka kuwa upekuzi na upatikanaji wa vipuli 101 ulitawaliwa na mashaka na ukiukwaji wa sheria.”

Majaji hao walisema kwa kuwa sababu hiyo pekee inatosha kumaliza rufaa hiyo, hawana sababu ya kuendelea kuchambua sababu zingine hivyo hukumu iliyomfunga kifungo cha miaka 30 inabatilishwa na mrufani aachiliwe huru.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *