
Dar es Salaam. Simba imepanga kurudi tena katika Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF kwa ajili ya kuomba kufanyike kwa marejeo ya shauri lao kumhusu mchezaji Mohamed Damaro.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescentius Magori amesema leo Jumanne, Aprili 7, 2026 kuwa Simba haijaridhishwa na uamuzi wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kutupilia mbali shauri lao juu ya uhalali wa uraia wa mchezaji huyo hivyo wanataka kufanyike marejeo ya shauri hilo kabla ya kwenda ngazi za juu zaidi.
“Tumepokea majibu ya kamati ya Hadhi, Sheria za Wachezaji. Tumeshaandaa marejeo ya mchezaji huyu na tutawasilisha hivi punde hapo TFF.
“Na katika hukumu ile waliyotupatia, imechagua tu maeneo yanayowafurahisha ndio wakajibu lakini maeneo mengine tuliyoyahoji hawajayajibu,” amesema Magori.
Magori amesema ameshangazwa kuona Damaro alipata uraia kwa haraka wakati wachezaji wa Simba walikataliwa.
“Mwaka jana na sisi tuliandika barua ya kubadili uraia wa wachezaji wetu lakini haijajibiwa hadi leo. Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa haipo kwenye mizania sawa sio japo sawa. Hili japo sio tu tunakwenda CAS lakini pia tunaiandikia FIFA. Kama mtu anapewa uraia ili tu achezee klabu pekee bila timu ya taifa ni jambo ambalo halikubaliki. Damaro hata ipite miaka 100 hawezi kucheza timu ya Taifa. Jambo lingine ambalo
TFF walitakiwa walifanye, kama kanuni zetu halizungumzii hilo basi wangetumia kanuni za juu kufanya maamuzi.
“Hili jambo sio ‘fair’ (sawa) sababu kuna timu moja ina wachezaji 13 kwa kutumia mlango wa nyuma. Na aliyedanganya mamlaka kwamba anapewa uraia ili acheze timu ya taifa basi alifanya udanganyifu mkubwa, unampa uraia wa nini tena mchezaji mwenyewe hana hata mwaka Tanzania. Ni jambo serious na sisi tupo nalo ‘serious’.
“Mashabiki wetu wametaharuki, wamekuwa na hasira, nafahamu mashabiki wetu wanakerwa na hili jambo na wanaona yanayotokea lakini niwasihi sana watulie. Sisi Simba ni timu ambayo inaweka mpira wa miguu mbele. Najua mpira una hasira kubwa. Bodi tunalishughulikia na tumeiandikia mamlaka, tutakutana nao na watatuambia kwanini hayo mamabo yanatokea mara kwa mara,” amesema Magori.
Aprili 2, 2026, TFF ilitangaza kutupilia mbali shauri lililokuwa limefikishwa mbele ya Kamati yake ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kuhusu uhalali wa Mchezaji Mohamed Damaro wa Yanga.
Klabu hiyo ilidai usajili wake umekiuka Kanuni ya 62(1) ya Ligi Kuu pamoja na Kanuni za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Kamati katika uamuzi wake, ilisema usajili wa Camara hauna dosari kwa vile habanwi na Kanuni zilizowasilishwa na klabu ya Simba.