
Wachezaji saba wa kikosi cha timu ya taifa ya mpira wa miguu ya Eritrea waliopata ushindi wa kihistoria huko Eswatini wiki iliyopita bado hawajarudi nyumbani huku wakiripotiwa kutoweka nchini Afrika Kusini.
Baadhi ya wachezaji wenzao wakiwa wamerejea, inasemekana wengine saba walitoroka wakati walipokuwa kambini.
Kumekuwa na visa kadhaa ambapo wachezaji kutoka Eritrea wanaoshiriki katika michezo mbalimbali wamekuwa hawarudi nyumbani baada ya mechi za kimataifa katika miaka ya hivi karibuni.
Serikali ya Eritrea mara nyingi imekuwa ikikabiliwa na ukosoaji mkubwa kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu na ukandamizaji wa kisiasa. Hali hiyo imekuwa ikiathiri hata sekta ya michezo, hususan mpira wa miguu.
Habari za wachezaji hao kutoroka zitakuwa pigo kwa timu hiyo, ambayo, imetoka kupata ushindi wa jumla wa mabao 4-1 dhidi ya Eswatini ilikuwa ikisherehekea kurudi katika hatua za makundi za kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 19.
Ni wachezaji 10 pekee kati ya 24 waliokuwa na makazi yao Eritrea na ni wachezaji watatu tu kati ya hao, akiwemo nahodha wa timu hiyo Ablelom Teklezghi na wengine ni Nahom Tadese na Romel Abdu ambao tayari wameripotiwa kurejea Eritrea.
Ingawa haijulikani wazi wachezaji waliopotea wamekwenda wapi, ripoti zinasema baadhi yao wameonekana Afrika Kusini.
Wachezaji wengine waliotoroka ni pamoja na golikipa Kubrom Solomon na winga mkongwe Medhanie Redie.
Tangu mwaka 2009, zaidi ya wachezaji 60 wa Eritrea wameripotiwa kutoroka wakati wa michezo ya kimataifa. Hali hiyo imeilazimu Shirikisho la Soka la Eritrea kujiondoa mara kwa mara katika mashindano makubwa kama vile michezo ya kufuzu Kombe la Dunia na AFCON.
Kutokana na hofu hiyo, Eritrea haijashiriki mechi yoyote ya ushindani tangu mwaka 2019, kwa kuwa mamlaka zake zimekuwa na tahadhari kubwa kuruhusu timu kusafiri nje, ambako hatari ya wachezaji kutoroka huwa kubwa.
Vyombo vya habari vya serikali ya Eritrea vimekuwa kimya kuhusu kurejea kwa timu hiyo iliyoshinda, jambo ambalo kwa kawaida lingeambatana na shamrashamra za kuwakaribisha nyumbani.
Vyanzo vinasema maandalizi yalifanywa kwa ajili ya kuwapokea wachezaji hao lakini yalifutwa kufuatia habari za kutoweka kwao.