
Dar es Salaam. Wakati vita dhidi ya biashara haramu ikiendelea kushika kasi nchini, Kampuni ya Tanzania Breweries Limited (TBL) imeonya kuwa kusambaa kwa pombe haramu kunaendelea kuhatarisha afya ya wananchi, kudhoofisha uchumi na kuathiri ustawi wa biashara halali.
Kauli hiyo imekuja huku kampuni hiyo ikipongeza juhudi za Serikali katika kukamata na kuondoa bidhaa bandia sokoni, ikisema hatua hizo zinaonesha dhamira ya kulinda watumiaji na kuhakikisha ushindani wa haki.
Hata hivyo, TBL imeeleza kuwa ukubwa wa tatizo la pombe haramu bado ni mkubwa, likiwa limeendelea kuwa sehemu ya matumizi ya pombe nchini na kuwaweka watumiaji wengi katika hatari ya bidhaa zisizo salama na zisizodhibitiwa.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, athari za kiafya zinazotokana na pombe haramu ni kubwa, ikiwemo uharibifu wa viungo vya mwili, kupoteza uwezo wa kuona na hata vifo. Katika baadhi ya jamii, madhara hayo tayari yameonekana wazi, huku wananchi wengi wakigusa moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja athari zake.
Mbali na afya, uchumi nao unaathirika. Inakadiriwa kuwa Tanzania hupoteza zaidi ya Sh1 trilioni kila mwaka kutokana na mapato yasiyokusanywa yanayohusiana na biashara ya pombe haramu. Fedha hizo, kwa mujibu wa wadau, zingeweza kuelekezwa katika kuboresha huduma za jamii kama afya, elimu na miundombinu.
Pia, biashara hiyo imekuwa kikwazo kwa ushindani wa haki sokoni. Wazalishaji wanaofuata sheria hulazimika kushindana na wafanyabiashara haramu wanaouza bidhaa kwa bei ya chini kutokana na kukwepa kodi na viwango, hali inayopunguza uwekezaji na kuathiri ajira katika mnyororo mzima wa thamani.
Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Michelle Kilpin amesema kuwa kukabiliana na changamoto hiyo kunahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, sekta binafsi na jamii.
Amesema pamoja na kuimarisha utekelezaji wa sheria, ni muhimu kuwepo kwa mifumo thabiti ya udhibiti, sera za kodi zinazotabirika pamoja na kuongeza uelewa kwa watumiaji na wauzaji kuhusu madhara ya pombe haramu.
“Mapambano dhidi ya pombe haramu hayawezi kufanywa na upande mmoja pekee. Ni jukumu la pamoja kuhakikisha bidhaa zisizo salama hazipati nafasi sokoni na watumiaji wanapata elimu ya matumizi salama,” amesema.
Licha ya hatua zinazoendelea kuchukuliwa, TBL imeonya kuwa upatikanaji rahisi na bei nafuu ya pombe haramu vinaendelea kuchochea matumizi yake, hasa kwa makundi ya kipato cha chini, hali inayohitaji mikakati ya muda mrefu na endelevu.
Kadri juhudi za kupambana na biashara haramu zinavyoendelea, wadau wanasema kipaumbele kinapaswa kuwa kulinda afya ya wananchi, kuhakikisha ushindani wa haki na kujenga soko la pombe lililo salama na lenye tija kwa uchumi wa taifa.