RAIS wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan amepokeo gawio la Sh.bilioni 15 kutoka Kampuni ya Kuhifadhi Mafuta Tanzania (TIPER) ikiwa ni sehemu ya gawio la Shilingi bilioni 30 lilitolewa na kampuni hiyo kwa wanahisa wawili wa kampuni hiyo.
Serikali inamiliki asilimia 50 ya TIPER na Oryx Energies nayo inamiliki asilimia 50 ya hisa za kampuni na gawio hilo kwa upande wa Serikali limekabidhiwa kwa Rais Samia.
Akizungumza katika hafla ya Siku ya Gawio Ikulu jijini Dar es Salaam mbele ya Rais Samia, Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu amesema TIPER mwaka huu imekuwa ni miongoni mwa kampuni zilizofanya vizuri na kuwa katika orodha ya kukabidhi mfano wa hundi ya gawio kwa Rais Samia.
“TIPER mwaka huu wameweza kuchangia gawio la sh. bilioni 15 na mwaka 2025 hawakukidhi viwango.Ni gawio kubwa kuwahi kutokea kutolewa na TIPER,” amesema Mchechu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TIPER, Mohamed Mohamed alisema kukabidhiwa wa gawio hilo ni kiwango kikubwa zaidi katika historia ya kampuni hiyo, akieleza mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa katika miundombinu, ufanisi wa uendeshaji na usimamizi madhubuti wa rasilimali.
Alisema mafaniko hayo yaliyopatikana pia yamechangiwa na kiasi kikubwa na mazingira rafiki ya uwekezaji yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya sita chini ya uongozi madhubuti wa Rais Dk Samia ambaye amekuwa akisisitiza uwekezaji wenye tija na matokeo chanya kwa Taifa.
Mohamed, alisema gawio ni sehemu ya faida ya kampuni inayorejeshwa kwa wanahisa baada ya kulipia gharama zote za uendeshaji, na kwa upande wa Serikali, fedha hizo huingia moja kwa moja Hazina Kuu kusaidia utekelezaji wa bajeti ya Taifa.
Akifafanua zaidi alisema kati ya mwaka 2016 na 2020 Serikali ilipokea gawio la jumla la Shilingi bilioni 7.65, lakini katika kipindi cha miaka mitano iliyofuata (2021–2025) gawio hilo liliongezeka zaidi ya mara nne na kufikia Shilingi bilioni 30.65.
“Ukuaji huu unaonekana wazi kwa kulinganisha gawio la Shilingi milioni 500 lililotolewa mwaka 2021 na gawio la Shilingi bilioni 15 lililotolewa mwaka 2025. Haya ni mafanikio makubwa ya kihistoria kwa TIPER,” alisema Mohamed.
Aliongeza pia mafanikio hayo yanamaanisha Watanzania wanapata manufaa ya moja kwa moja kupitia mapato ya Serikali yanayotumika kujenga barabara, hospitali, shule, kusambaza umeme vijijini na kugharamia huduma nyingine muhimu za kijamii.
“Kwa kufanya biashara yenye faida, TIPER inachangia kuongeza mapato ya Serikali, kupunguza utegemezi wa kodi kutoka kwa wananchi na kusaidia kugharamia huduma muhimu zinazoboresha maisha ya Watanzania,” alisema.
Alisema TIPER ilianzishwa mwaka 1966 kama kiwanda cha kusafisha mafuta ghafi kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na AGIP ya Italia, lakini mwaka 2000 ilibadili shughuli zake na kuwa kituo cha kuhifadhi mafuta kwa wingi baada ya shughuli za usafishaji kuonekana kutokuwa na tija kiuchumi.
“Kwa sasa kampuni hiyo inamilikiwa kwa ubia wa asilimia 50 kwa Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina na asilimia 50 kwa Oryx Energies Tanzania, ushirikiano ambao umechanganya maslahi ya umma na utaalamu wa sekta binafsi,” alisema.
Akieleza zaidi alisema katika kipindi cha miaka 10 iliyopita TIPER imewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 105 katika kuboresha miundombinu muhimu, ikiwemo matangi ya kuhifadhi mafuta, mifumo ya usambazaji wa mafuta, mifumo ya kuzima moto pamoja na mifumo ya umeme .
Aidha, aliongeza uwezo wa kuhifadhi mafuta kutoka lita milioni 253 hadi milioni 313, pamoja na kujenga kituo kipya cha kisasa cha kupakia mafuta kwenye malori.
Aidha, alisema kuanza kwa mfumo wa Single Receiving Terminal (SRT) wa mafuta ya Dizeli Januari 2025 kumeongeza ufanisi wa shughuli za bandari kwa kupunguza muda wa meli kupakua mafuta kutoka wastani wa siku tisa hadi siku nne, hatua iliyopunguza gharama za ucheleweshaji wa meli na kuongeza idadi ya meli zinazohudumiwa kila mwezi.
Mohamed alieleza kuwa tofauti na kampuni zinazouza mafuta moja kwa moja, TIPER hupata mapato kutokana na huduma za kuhifadhi na kusafirisha mafuta, hivyo mabadiliko ya bei za mafuta duniani hayaathiri kwa kiwango kikubwa faida ya kampuni.

Kutokana na nafasi ya kimkakati ya Tanzania katika kusambaza mafuta kwa nchi jirani zisizo na bandari, ikiwemo Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Cong (DRC)o, Rwanda, Burundi, Uganda na Malawi huku mahitaji ya huduma za TIPER yanaendelea kuongezeka.
Pia alisema kuwa kampuni imeandaa mpango wa kuwekeza zaidi ya Shilingi bilioni 265 katika kipindi cha miaka mitano ijayo ili kuongeza uwezo wa kuhifadhi, kupokea na kusafirisha mafuta, hatua itakayoimarisha usalama wa nishati nchini na kuiweka Tanzania kuwa kitovu cha biashara ya mafuta katika Afrika Mashariki na Kati.
“Kadri uchumi wa Tanzania unavyoendelea kukua na idadi ya watu kuongezeka, mahitaji ya nishati yanaendelea kuongezeka pia.
“Hatua yetu inayofuata ni kukamilisha ujenzi wa miundombinu mipya ili kuongeza zaidi uwezo wetu wa kuhifadhi mafuta na kuyasafirisha kwa haraka zaidi,” alisema.