SERIKALI imeeleza dhamira yake ya kufufua zao la kahawa nchini, ikilitambua kama “dhahabu ya kijani” kutokana na mchango wake katika kuinua uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia maendeleo ya mazao na usalama wa chakula, Prof. Peter Msofe, amesema hayo wakati wa uzinduzi wa ugawaji wa miche ya kahawa uliofanyika katika Kata ya Uru Mashariki, Wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro.
Amesema serikali imejipanga kuhakikisha zao la kahawa linafufuliwa ili kurejesha heshima na mchango wake katika maisha ya wananchi, akibainisha kuwa kahawa bora nchini huzalishwa katika mkoa huo. Hapo awali, Prof. Msofe amesema kahawa ilikuwa nguzo kuu ya uchumi wa Kilimanjaro, ikiwezesha wananchi kugharamia elimu ya watoto na kuendesha maisha yao ya kila siku, na kuongeza kuwa hata yeye binafsi amenufaika na zao hilo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tanzania Coffee Board (TCB), Primus Kimaryo amesema utafiti wa muda mrefu umewezesha kupatikana kwa miche bora ya kahawa itakayoongeza uzalishaji iwapo itatunzwa ipasavyo.SOMA: Wakulima Kilimanjaro waonywa ung’oaji miche ya kahawa
Amesema kahawa ni urithi waliopokea kutoka kwa mababu zao, lakini kupitia juhudi za serikali na wadau mbalimbali, zao hilo linaelekea kuwa zao la kibiashara lenye tija kubwa zaidi. Ameongeza kuwa wakulima wanaweza kujinasua na umaskini iwapo watatumia vizuri ardhi yao kwa kufuata maelekezo ya kilimo bora na kuzalisha kahawa yenye ubora itakayouzwa kwa faida kubwa.
