Katika taarifa iliyotolewa tarehe 9 Aprili 2026 mjini New York, Marekani, UNICEF imesema mashambulizi hayo dhidi ya wapiganaji wa Hezbollah kusini mwa Lebanon yamesababisha makumi ya watoto kiupoteza maisha au kujeruhiwa ndani ya muda mfupi.
Watoto waathirika wakubwa wa mashambulizi
UNICEF imeeleza kuwa katika siku ya hivi karibuni pekee, mashambulizi ya anga yameripotiwa kusababisha vifo vya watoto 33 na kujeruhi wengine 153 nchini humo. Hali hiyo inaongeza idadi ya watoto waliouawa au kujeruhiwa kufikia takribani 600 tangu tarehe 2 Machi 2026.
Aidha, shirika hilo limepokea taarifa za watoto kunasuliwa kwenye vifusi, huku wengine wakiwa bado hawajulikani walipo au wametenganishwa na familia zao. Watoto wengi wanakabiliwa na mshtuko wa kisaikolojia baada ya kupoteza wapendwa wao, makazi na hali ya usalama.
Mamilioni wakimbia makazi yao
Kwa mujibu wa UNICEF, zaidi ya watu milioni moja wamelazimika kuyakimbia makazi yao nchini Lebanon, wakiwemo takribani watoto 390,000. Wengi wao wamekumbwa na hali hiyo mara kadhaa, baadhi yao wakiyakimbia makaazi yao kwa mara ya pili, tatu au hata nne kutokana na kuendelea kwa mapigano.
UNICEF inasambaza vifaa vya shule kwa familia zilizohamishwa nchini Lebanon Kusini.
Wito wa kulindwa kwa raia
UNICEF imesisitiza kuwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu, raia wote, hususan watoto, wanapaswa kulindwa wakati wote. Imevitaka pande zote zinazohusika katika mgogoro huo kuchukua tahadhari zote zinazowezekana kulinda raia na miundombinu ya kiraia, pamoja na kuhakikisha upatikanaji salama na endelevu wa misaada ya kibinadamu.
Shirika hilo limeonya kuwa matumizi ya silaha zenye madhara makubwa katika maeneo yenye msongamano wa watu yanaweka maisha ya watoto hatarini zaidi.
Hatua za dharura za UNICEF
UNICEF inaendelea kutoa msaada wa haraka nchini Lebanon, ikiwemo kuwahudumia watoto waliojeruhiwa kupitia programu ya kusaidia watoto walioumia na kuathiriwa na vita. Pia, shirika hilo linaongeza juhudi za kusambaza vifaa muhimu katika makazi ya wakimbizi, kutoa dawa katika vituo vya afya, na kuendesha huduma za matibabu kupitia timu za simu kwa familia zilizohamishwa.
Wito wa amani na hatua za haraka
UNICEF imeonya kuwa licha ya jitihada za kusitisha mapigano katika maeneo mengine, hali ya Lebanon bado ni hatarishi na inaweza kudhoofisha juhudi za kufikia amani ya kudumu katika ukanda huo.
Shirika hilo limesisitiza kuwa watoto wa Lebanon hawawezi kuachwa nyuma, na kutoa wito kwa hatua za haraka kuhakikisha ulinzi wao na ustawi wao katika kipindi hiki cha mgogoro.