DAR ES SALAAM: Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imesema Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yamekuwa jukwaa muhimu la kuhamasisha utalii wa ndani, kutangaza vivutio vya utalii na kuwaandaa wadau kunufaika na fursa mbalimbali ikiwemo mashindano ya AFCON yanayotarajiwa kufanyika mwaka ujao.

Akizungumza katika maonesho hayo Naomi Mbilinyi, Ofisa Utalii Mwandamizi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), amesema jukumu la TTB ni kutangaza utalii wa Tanzania ndani na nje ya nchi, na kwamba Sabasaba imekuwa sehemu muhimu ya kuwafikia wananchi na wadau wa sekta hiyo.

Amesema kupitia banda la TTB, wananchi wanapata taarifa kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya utalii, ikiwemo namna ya kuanzisha kampuni za utalii, kushiriki maonesho ya kimataifa na kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo nchini.

Mbilinyi ameeleza kuwa TTB pia inatumia maonesho hayo kutangaza Swahili International Tourism Expo, yatakayofanyika mwezi Oktoba, ambapo wadau wanapata fursa ya kujisajili kama waoneshaji, wadhamini na washiriki wa maonesho hayo ya kimataifa.

Aidha, amesema bodi hiyo inaendelea kujenga mfumo wa kidijitali utakaowezesha wadau wa utalii kusajili taarifa za biashara zao ili kutangaza huduma na vivutio vyao kwa urahisi katika masoko ya ndani na nje ya Tanzania.

Kwa mujibu wa Mbilinyi, banda la TTB pia limetenga eneo maalum la kutoa elimu kuhusu fursa zitakazotokana na mashindano ya AFCON, likiwaelimisha watoa huduma za malazi, usafiri na sekta nyingine jinsi ya kujiandaa kupokea wageni wengi watakaoingia nchini wakati wa mashindano hayo.

Amesema wageni wengi wanaotembelea banda hilo, hususan wakazi wa Dar es Salaam, huonyesha hamu ya kujifunza kuhusu maeneo ya utalii yaliyo karibu nao, ikiwemo fukwe, maeneo ya kihistoria, makumbusho na vivutio vingine vinavyoweza kutembelewa kwa safari za siku moja (city tour).

Pia amesema wananchi wengi huulizia gharama za kutembelea hifadhi za taifa na maeneo mengine ya utalii, ambapo TTB hushirikiana na taasisi mbalimbali za sekta hiyo kuwapa taarifa sahihi na kuwaelekeza kwenye mabanda husika.

Ametoa wito kwa wananchi, Mbilinyi aliwahimiza kutembelea banda la TTB katika Maonesho ya Sabasaba ili kupata taarifa mbalimbali ambazo si rahisi kuzipata sehemu nyingine, ikiwemo usajili wa mifumo ya kidijitali, taarifa kuhusu Swahili International Tourism Expo na maandalizi ya AFCON.

Amesisitiza kuwa maonesho hayo yanatoa nafasi ya wananchi kuzungumza moja kwa moja na wataalamu wa utalii, kuuliza maswali, kutoa maoni na kupata mwongozo kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya utalii nchini.£

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *