Akizungumza kutoka Beirut, Mji mkuu wa Lebanon ambako alishuhudia moja kwa moja mashambulizi ya juzi Jumatano, mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO), Abdinasir Abubakar, amesema kulingana na takwimu za hivi karibuni kutoka Wizara ya Afya ya Lebanon, takriban watu 300 waliuawa katika mashambulizi hayo ikiwa ni miongoni mwa idadi kubwa zaidi ya vifo katika siku moja tangu kuanza kwa mapigano kati ya Israel na Hezbollah tarehe 2 Machi na watu 1,150 walijeruhiwa.
“Watu wengi zaidi bado hawajapatikana… inaaminika wako chini ya vifusi,” anasema Dkt. Abubakar na kwamba bado wana miili mingi ambayo haijatambuliwa na wanasubiri itambuliwe.
Dkt. Abdinasir Abubakar, Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Lebanon, anawasiliana na watoto katika uwanja wa michezo mjini Beirut.
Anaeleza kuwa hospitali zimeelemewa, zikifanya kazi kupita uwezo wake, huku madaktari wakikabiliwa na hatari inayoongezeka. Kuna hofu hata kwamba magari ya wagonjwa yanaweza kulengwa.
“Wahudumu wa afya, vituo vya afya na magari ya wagonjwa vinalindwa chini ya sheria za kimataifa,” anasisitiza na kwamba bila huduma hizi, hawataweza kuokoa maisha.”
Kwa raia nchini Lebanon, kuishi sasa kunamaanisha kukimbia tena na tena. Familia ambazo tayari zilikuwa zimekimbia vurugu za awali sasa zinalazimika kuhama kwa mara nyingine, zikiwa na watoto, kumbukumbu na mali chache walizobaki nazo. Maeneo yaliyokuwa yakionekana salama yalishambuliwa ghafla, na kusababisha hofu na kuwafanya watu kukimbia kwa mara ya pili au ya tatu.
Kwa upande wa Sudan, mgogoro wa muda mrefu na ambao hauangaziwi sana unaendelea kuingia katika kina kirefu zaidi, mwaka wa nne. Akiwa katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum kwa njia ya video Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR nchini Sudan, Marie-Helene Verney amewaelezea waandishi wa habari jijini Geneva, Uswisi, jinsi Sudan inavyokumbwa na uhamaji wa mara kwa mara.
Wakimbizi wa Sudan wamekusanyika katika makazi ya muda huko Koulbous, Chad, karibu na mpaka wa Sudan baada ya kukimbia vita vinavyoendelea. (Maktaba)
Anasema, “robo ya Wasudan wote wamefurushwa tangu kuanza kwa mapigano. Hiyo ni takribani watu milioni 14 na kwamba wakati anaongea kuna takribani watu milioni 12 ambao bado wameyakimbia makazi yao, milioni nne kati yao wakiwa kati nchi jirani kama Chad, Sudan Kusini na Misri.”
Ameeleza kuwa takwimu zinaonesha mtu mmoja kati ya wanne nchini Sudan amefurushwa kutoka nyumbani kwake. Mamilioni ya watoto wamekua bila elimu au utulivu, na wengi wametenganishwa na familia zao. Wanawake na wasichana wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi za ukatili na unyanyasaji wanaposafiri katika maeneo yasiyo salama.