Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, leo Ijumaa, Aprili 10, 2026 ametangaza kusimamisha Mchakato wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC).

Uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Jumapili, Aprili 12, 2026 hapa Dar es Salaam ambapo nafasi za Rais, Makamu wa Rais na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji zingewaniwa.

Sababu ya Waziri kusimamisha mchakato huo ni kufuatia malalamiko ya baadhi ya wagombea waliokuwa wakiwania nafasi mbalimbali za uongozi wa TOC kuenguliwa kushiriki katika uchaguzi huo.

Mbali na kusimamisha Uchaguzi huo, Makonda ameunda kamati ya muda ya uongozi yenye Wajumbe saba wakiongozwa na Mwenyekiti Ismail Aden Rage na Makamu Mwenyekiti, Dk. Steven Mabagala.

Amechukua hatua hiyo kwa mamlaka aliyonayo Kisheria ya kusimamia sekta ya michezo nchini, ikiwemo Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995 na Sheria za Baraza la Michezo la Taifa Sura ya 49 ambazo zinampamamlaka ya kusimamia utekelezaji wa Sera na kuhakikisha taasisi zote zilizo chini ya Sekta ya Michezo zinaendeshwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na misingi ya utawala bora.

Halikadhalika, Waziri Mwenye dhamana ya michezo ana wajibu wa kulinda haki za wanachama wa vyama vya michezo na kuhakikisha usawa na uwazi unazingatiwa wakati wote.

“Serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuweka mazingira bora yaMaendeleo ya Michezo nchini ili kuhakikisha Tanzania inashiriki kikamilifu na kwa mafanikio katika mashindano ya Kimataifa kama vile Michezo ya Jumuiya ya Madola, Michezo ya Afrika na Michezo ya Olimpiki..

“Ni matarajio yangu kuwa kupitia uamuzi huu, Kamati ya Olimpiki Tanzania itaimarika zaidi na kuweka mazingira bora yatakayowezesha Wanamichezo wetu kufanya vizuri Kimataifa na hatimaye kuliletea Taifa heshima kwa kushinda medali, hususan Medali za Dhahabu ambazo zimekuwa adimu kwa muda mrefu.

“Ninawaomba wadau wote wa michezo kuwa watulivu, kuendelea kushirikiana, na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya Uchunguzi na Uongozi wa muda ili kufanikisha mchakato huu wa marekebisho kwa manufaa ya Taifa,” amesema Waziri Makonda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *