Dar es Salaam. Ni wazi kuwa tasnia ya filamu Bongo imeendelea kupitia mabadiliko kila kukicha. Kutoka kule kwenye single movie zilizokuwa zikiuzwa katika mfumo wa CD hadi sasa ambapo kumeenea tamthilia kila kona.

Nyuma ya mafanikio ya mabadiliko hayo wapo wanaopambania kuhakikisha gemu ya filamu inavuka mipaka na kuleta manufaa. Kati ya watu hao yupo Simon Cherehani, mwandishi wa skripti, mwongozaji na mzalishaji wa filamu Bongo anayekuja kwa kasi.

Akizungumza na Mwananchi Cherehani ambaye  ni Mkurugenzi wa kampuni ya Dreamspace Studios amesimulia safari yake hadi kufikia kufanya kazi na watu maarufu kama Phina, Eni, Irene Paul, Patric Kanumba na wengine.

“Nilianzia kwenye uandishi wa habari nimesoma Dar es Salaam School of Journalism (DSJ) nilisoma hivyo kwasababu zamani ilikuwa hakuna sehemu wanafundisha filamu ilikuwa inafundishwa kama somo ndani ya Journalism. 

“Nilitoka form 6 nikaingia Diploma mwaka 2019 niliwaongopea wazazi wangu nimeenda UDSM. Bahati nzuri Mungu akasaidia baada ya mwezi mmoja nikapata kazi Clouds,” amesema Cherehani. 

Amesema  wakati yupo chuo akichukua warembo na kuwatafutia michongo kwenye video za muziki na matukio mbalimbali kisha kugawana malipo baada ya kazi.

“Nilikuwa nachukua hata wadada sita nawapeleka kwenye video halafu wakipata hela tunakatana. Nikawa nawapeleka na kwenye kampuni chuoni wakawa wanaona  nina konesheni.

“Sasa Clouds walipoanza kutafuta watu na mimi nikapata upenyo walikuwa wanafungua TV yao ilikuwa inaitwa Clouds Plus. Nikapata kipindi nikiwa bado nasoma,” anasema.
Cherehani ameeleza kuwa katika kipindi hicho alichopata  alikuwa  akikizalisha, akihariri kisha mtu mwingine alikuwa akimalizia uhariri wa mwisho.

“Baadaye nikawaambia wazazi kuwa nimechaguliwa kufanya kazi, ila nikawaambia ukweli kuwa niliwadanganya sikufaulu kwenda UDSM. “Nakumbuka mshahara wangu wa kwanza ulikuwa laki tano, nilimtumia mama laki nne mimi nikabaki na moja nikatuma laki nne nikabaki na moja nilikuwa bado sina majukumu,” anasema Cherehani.

Amesema maisha ya utangazaji kwenye TV hayakumvutia kutokana na mitazamo ya watu.

“Nilikuwa nikitembea mtaani watu wanasema nguo niliyovaa niliivaa kwenye kipindi cha jana, nikaona kero. Nikawa tena sipendi kukaa kwenye TV.  Nilikuwa nataka kukaa nyuma ya kamera nikaja kukutana na Lamata.

Alivyokutana na Lamata

Cherehani anasema alikutana na Lamata  kipindi akiwa anajiandaa kufanya tamthilia ya Kapuni.

“Rafiki yangu alikuwa ameniita kwenye seti yao kwa ajili ya kuangalia. Nilipofika pale sikujali kama nimeajiriwa nikaanza kusaidia kwenye mapungufu. Lamata akaniona akaniuliza kama nafanya kazi pale nikamwambia mimi nasaidia akaniambia anataka niwe kwenye timu yake. 

“Sikumwambia kuwa nipo Clouds nikawa najigawa Shule, Lamata na Clouds. Kuna siku boss wangu wa Clouds alikuwa anaitwa Ramadhan akanipigia simu kuniita, nikaulizwa kwanini siendi ofisini nikadanganya sina kodi, akalipa akauliza kingine nikamwambia sina mkataba akaniambia kesho tukutane,”anasimulia Cherehani.

Tunaweza kusema michongo iligongana kwani Lamata nae alitaka kuingia mkataba na Cherehani.

Alivyompeleka Dora kwa Lamata

Anasema wakati harakati za kusaini mkataba zikiendelea alikutana na Dorah wa kwenye Jua Kali.

“Bahati nzuri hicho ndio kipindi namuona Dorah chuo, nilikuwa nimemuacha kama madarasa mawili nikawa nimepata hisia kwamba huyu mbona tunaweza kumwingiza kwenye biashara. Nakumbuka nilikuwa nataka nimpeleke Shilawadu lakini nikabadili uamuzi usiku nikampeleka kwa Lamata.

“Dora alikuwa hataki, akaniambia nisimpeleke kwa Lamata alikuwa hata hajui Kinondoni ni wapi nilimpandisha gari akiwa anajua anaenda Mikocheni kumbe alikuwa anaenda Sinza. inatakiwa kutengeneza uthamani na kumfanya mtu ajikubali. 

“Lamata akaanza kuniamini nikaenda kwa boss Rama akaniambia tunasaini mkataba akaniambia nitalipwa laki saba ikiwa tayari imekatwa makato hapo ilikuwa hela kubwa kwangu. Lamata nae  akasema atakuwa ananipa laki tatu kwa mwezi,” anasema Cherehani.

Kwasababu alijua ndoto anazozifukuzia Cherehani alikataa kusaini mkataba wa laki saba, badala yake alienda kwa Lamata ambapo alikuwa akilipwa laki tatu.

“Tulivyofanya kazi na Lamata kila baada ya msimu pesa inapanda mpaka mwaka unaofuata mshahara ulipanda mpaka milioni nne nilifanya kazi kuanzia 2021 hadi 2024, anasema.

Licha ya mshahara wake kuongezeka anasema alikuwa anaona bado kuna kitu kinapungua.

“Nakumbuka siku moja nimepanda ndege naenda Mwanza nikakutana na jamaa akawa ananiuliza maswali kuhusu Bongo Movie  kwanini tasnia haikui nikampa sababu zangu.

Akanionesha movie akaniuliza  kama naweza kufanya kama hiyo kisha akaniambia nikirudi Dar tuonane.

“Alivyorudi tukaonana kumbe alikuwa anaandika listi ya vitu nilivyokuwa namtajia nilimkuta na kamera tatu kama zile nilizomtajia. Halafu akaanzisha application. Akasema anataka nimfanyie movie bahati mbaya nikamwambia nimeajiriwa,” anasema.

Baada ya  kushindwa kufanya kazi na sehemu hiyo, aliombwa kutafuta watu wa kufanya hivyo yeye atasimamia tu.

Alivyotimuliwa kwa Lamata

“Kuna kipindi  nilikuwa napitia jambo, nilikuwa nategemea mtoto na  mtu ambaye sijaoana nae na alikuwa kwa wazazi wake. Nilikuwa mpaka kazini napata usingizi, boss (Lamata) akawa anaona sipo sawa akawa anauliza kama nakesha kwenye kazi nyingine.

“Siku moja akanikuta nimelala katikati ya kazi akanifuata akaniambia kuanzia leo ni mwisho kufanya kazi na wao. Akahisi kuna sehemu nafanya kazi hakujua kumbe nilikuwa na mawazo,” anasema.

Baada ya kutimuliwa ndipo alirudi kwa jamaa aliyekutana naye kwenye ndege na kisha kufanya nae kazi.

“Hapo ikawa safari yangu na kazi yangu ya kwanza ku-direct mwenyewe na ku-produce ilifanyiwa promotion lakini ilikuwa kwenye application ambayo watu sio rahisi kuipata  nikawaza kitu kipya cha kuja nacho.

“Nikakutana na Othman Njaidi (Patric Kanumba) akawa anataka kufanya kazi yake mwenyewe. Nikamwambia tuanze kazi tukatafuta hela tukafanya Situationship ambayo humo ndani ikamtambulisha Prisca Limo ambaye watu walikuwa hawamfahamu lakini humo ndani wakaanza kumjua,” anasema.

Ameitaja Situationship kama kazi yake iliyomfungulia milango zaidi

“Situationship ikafanya nikaenda Kenya na kupata mialiko ya kwenye filamu na hata Eni (rafiki wa mke wa Jux) akapata nafasi ya kuni- DM akaomba tufanye kazi,” anasema Cherehani.

Ndiye aliyewakutanisha Eni na Phina

Kazi ikaanza kati ya Eni na Cherehani ambapo anasema mwanzo Eni aliomba majina ya wadada watatu ili afanye nao kazi.

“Nilimpa list alikuwapo  Ruby, Abigail  Chams na Cherry Cherry,  Phina hakuwapo. Nilichukua link ya Ruby akiwa anaimba kanisani nikamtumia Eni akapenda sana Ruby anavyoimba akaomba ajue namna ya kumpata ili wafanye project.

“Likaja suala la gharama Ruby alitaja kiasi chake ambacho kwa Eni hakikuwa sawa. Maana Eni alitaka wafanye collaboration kila mmoja aweke nguvu yake ila atamsaidia kupata kolabo za Nigeria. Alivyoona Ruby kataja hela ndefu akataka mwingine nikamtumia Phina,” anasema.

Anaendelea; Eni na Phina waliendana na kuelewana kwa haraka ndipo wakaanza kazi. Hata hivyo kuhusu wawili hao kuwa kwenye uhusiano Cherehani anasema hajui chochote.

“Nikaona ukaribu kati yao kwahiyo mengine ni wao kwasababu hata nikienda kwenye apartment ya Eni namkuta Phina. Ila hawajawahi kujitambulisha kwangu na hata suala la pesa nikimwomba Eni, Phina ndiyo anashughulika.

“Zamani Eni akija Tanzania alikuwa ananipigia simu lakini siku hizi Phina ananipigia mbona huji kumuona Eni. Zile video unazoona anafanya na Phina  mimi ndio huwa na-direct kazi nzuri huwa inajitangaza,” anasema Cherehani. 

Alivyotengwa

“Nilivyoachishwa kazi kwa Lamata nilitengwa. Watu wote hawakuwa upande wangu karibia crew nzima ambao nilikuwa nawaona washikaji. Kipindi naanza kujitegemea nilikuwa sina makazi lakini hakuna mtu alikuwa najua nilikuwa nalala kwa mshikaji,” anasema

Wanasema tabasamu huficha huzini Cherehani anasema kuna wakati alikuwa anapitia magumu lakini yalifichwa na tabasamu.

“Mikocheni nilikuwa nakaa nyumba nzima nilivyoachishwa kazi jukumu likaenda kwa mtoto  nikawa hela nyingi zinaenda huko. Sehemu ambayo nilikuwa naishi ilikuwa inauzwa kwa hiyo mwenye nyumba alinipa miezi ambayo nilikaa bure.

“Nikawa sijatafuta hela ya maana ya kodi na hela  ilitakiwa iende kwenye uzinduzi ilibidi niweke hela ili nipate hela. Kwenye uzinduzi nimepiga suti nacheka naongea kumbe nakaa kwa rafiki,” anasema Cherehani.

Ushauri kwa vijana

“Sisi ni vijana tunajisahau tunaendeleza kujenga ambavyo tumevikuta tunasahau kujenga vyetu vijana tujitengenezee utamaduni wa kujenga vya kwetu,” anasema.

Hata hivyo ametaja sababu za yeye kufanya kazi nyingi na vijana.

“Ninaamini vijana tunachukuliwa poa sana kama wapenda starehe sio wabunifu. Vijana wanasahaulika  hata kwenye fursa unaweza kuwa na sifa lakini usipate nafasi mimi nilivyokuja kuingia kwenye industry niliko waigizaji wakongwe nikiwaita watanidharau.

“Wameniona natumwa naagizwa soda nikaona nichukue vijana wapya ndio maana nikatengeneza  story ambazo zinagusa vijana,” anasema.

Ikumbukwe Cherehani ndiye aliyemtengeneza mwigizaji Anna Nyange ambaye hivi karibuni pia alionekena kwenye wimbo wa Harmonize na Mbosso ‘Leo’ akiigiza kama mpenzi wa Harmonize.
Akimalizaa Cherehani amesema hivi karibuni kutakuwa na kazi mpya ambayo ndani yupo mwigizaji mkongwe Irene Paul.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *