Dar es Salaam. Wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji nchini wametakiwa kulipa kodi kwa uaminifu ili kuifanya nchi kujitegemea kupitia mapato yake ya ndani katika kipindi hiki cha mabadiliko makubwa ya kiuchumi yanayoendelea duniani, ikiwemo kupungua kwa misaada.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Rais Samia Suluhu Hassan Julai 1, 2026 katika hafla ya ugawaji wa Tuzo ya Rais kwa Mlipakodi, iliyoenda sambamba na maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mwaka 1996.
Rais Samia amesema anatamani kuwe na wigo mpana wa walipakodi wazalendo wanaojua wajibu wao, pamoja na watendaji wa TRA watakaozidisha weledi, ubunifu na uadilifu ili wamwachie alama nzuri atakapoondoka madarakani mwaka 2030.
“Sote ni mashahidi wa mabadiliko na mwelekeo wa siasa za dunia kila kukicha na mabadiliko haya yanaathiri nyanja zote za maisha, ikiwemo kushuka kwa uchumi kunakoonekana katika mataifa mengi duniani kwa wakati huu.
Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia kwenye maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.
“Tunaishi kwenye zama za mataifa kukabiliana katika biashara na, kwa kiasi kikubwa, kupungua kwa misaada, zama za kuongezeka kwa masharti ya mikopo, wakati huohuo kukiwa na ongezeko la uhitaji wa wananchi,” amesema.
Amesema kwa msingi huo hakuna budi kujenga uwezo wa ndani kwa kuimarisha ukusanyaji wa mapato ili kujenga uchumi wa kujitegemea kwa kiasi kikubwa kwa kutumia mapato ya ndani.
“Kulipa kodi ni wajibu, uzalendo na kutunza heshima ya taifa letu katika kuelekea kujitegemea. Taifa lolote ili liwe na nguvu ya kupanga, kuamua na kutekeleza mipango ya maendeleo yake halina budi kujenga mfumo imara wa kodi na mapato ya ndani wenye ufanisi na kuaminika, na hivi ndivyo wenzetu walioendelea walivyofikia hatua hiyo,” amesema.
Rais Samia amesema hayo wakati makusanyo ya TRA yakiongezeka mwaka hadi mwaka.
Kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, mamlaka hiyo kwa Tanzania Bara na Zanzibar imefanikiwa kukusanya Sh37.9 trilioni kuanzia Julai 1, 2025 hadi Juni 30, 2026, ikivuka lengo la makusanyo ya Sh36.6 trilioni. Hilo ni ongezeko kutoka Sh32.2 trilioni zilizokusanywa mwaka uliopita.
Mkuu huyo wa nchi amesema kodi zinazokusanywa, sambamba na vyanzo vingine vya mapato ya Serikali, ndizo zinazoendesha huduma za jamii na kwa kiasi kingine kuendesha miradi ya maendeleo.
Rais Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo ya Heshima ya TRA katika kumbukizi ya miaka 30 ya Mamlaka ya Mapato Tanzania kwenye hafla iliyofanyika Julai1, 2026 katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.
Kutokana na hilo, amesisitiza kuwa kulipa kodi ni wajibu wa kila mmoja katika kujenga taifa linalojitegemea kwa kuwa ndiyo nguzo imara ya kujitegemea.
Rais Samia amesema anatamani kuwe na wigo mpana wa walipakodi wazalendo wanaojua wajibu wao, mifumo iliyorahisishwa, pamoja na watendaji wa TRA watakaozidisha weledi, ubunifu na uadilifu.
Amesema hatua hiyo itaifanya TRA kukusanya kiasi kikubwa zaidi cha mapato katika kuelekea kujitegemea kama nchi kupitia mapato ya ndani na vyanzo vingine vya Serikali, jambo linalotegemea walipakodi na mamlaka hiyo.
“Natamani tukuze mifumo iliyorahisishwa na inayosomana ya ukusanyaji mapato nchini. Watendaji wazidishe weledi. Mkiyafanya hayo yote mtaniachia alama hata wakati nikimaliza muda wangu,” amesema.
Kwa upande wake, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, ameipongeza TRA kwa kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato huku akiahidi kutoa ushirikiano wa kutosha.
“Mafanikio tunayoyapata ya kuongezeka kwa kiwango cha ukusanyaji kila mwaka ni matunda ya uwajibikaji wa TRA, hivyo tuendelee kuongeza mikakati madhubuti ya kuendelea kukusanya mapato,” amesema.
Rais Samia Suluhu Hassan akisikiliza historia ya miaka 30 ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) baada ya kuwasili katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam Julai 1, 2026.
Katika hafla hiyo, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema kwa kuendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, mamlaka hiyo inapaswa kwenda sambamba na mabadiliko ya uchumi, uwekezaji unaoendelea na kuboresha utendaji katika kuhudumia uchumi wa nchi.
Maelezo ya TRA
TRA imesema inaendelea kujenga uhusiano bora na walipakodi nchini huku ikiendelea kuwa wabunifu na kutoa elimu ya kodi, kama alivyobainisha Kamishna Mkuu, Mwenda, katika hafla hiyo.
“Tutaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa watumishi bora, kuwafikia walipakodi sambamba na kutumia njia mbalimbali ikiwemo michezo, na ndiyo maana tuliamua kuanzisha klabu ya mpira ya TRA United.
“Tutaendelea kuhakikisha tunakusanya zaidi na kuifanya nchi yetu iendelee kiuchumi. Tutaendelea kuzuia upotevu wa mapato, kusimamia kodi za kimataifa, kuwa wabunifu sambamba na kutoa elimu ya kodi,” amesema.
Katika hafla hiyo, Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) ilitunukiwa tuzo mbili ikitambuliwa kuwa mlipakodi namba moja nchini na kampuni inayozingatia kwa kiwango cha juu zaidi sheria za kodi kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Akizungumzia tuzo hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Ashraf Suryaningrat alisema heshima hiyo ni matokeo ya juhudi za pamoja za wafanyakazi, wasambazaji na wadau wote wanaoshirikiana na kampuni.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akimkabidhi tuzo ya Mlipakodi Bora wa Jumla na Mchangiaji Bora wa Kodi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025, Mkurugenzi Mtendaji wa Geita Gold Mining Limited (GGML), Ashraf Suryaningrat, wakati wa hafla ya Tuzo za Rais za Walipakodi iliyofanyika Julai 1, jijini Dar es Salaam.
“Utambuzi huu unaakisi kazi kubwa inayofanywa na kila mfanyakazi wa Kitanzania, kila msambazaji na kila mshirika ambaye amechangia kufanikisha viwango hivi vya utendaji.
Sekta ya madini ina nafasi muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya Tanzania, na ulipaji wa kodi kwa uaminifu ni moja ya njia muhimu zaidi tunazotimiza wajibu wetu kwa taifa,” alisema.
Alieleza kuwa tuzo hizo zina umuhimu mkubwa katika muktadha wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo imeitambua sekta ya madini kuwa moja ya nguzo kuu za kufanikisha azma ya Tanzania kuwa na uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.