Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa leo Jumatatu tarehe 13 Aprili 2026, mashirika hayo yamesema Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) na Jeshi la Watu wa Sudan (SAF) vinaendelea kutekeleza mashambulizi makubwa dhidi ya raia kote nchini Sudan.

Maelfu wauawa katika vita vya kikatili

Tangu kuanza kwa mapigano katikati ya Aprili 2023, Mashirika hayo mawili yamesema makumi ya maelfu ya raia, pamoja na watu wasiokuwa vitani, wanaaminika kuuawa katika mgogoro huo unaoelezwa kuwa wa kikatili na unaokiuka wazi misingi ya sheria za kimataifa.

Ripoti hiyo ya pamoja inaeleza kuwa vita hivyo vimekuwa na ukatili wa kimfumo unaowaathiri vibaya wananchi wa kawaida.

Familia nchini Sudan ambazo zimekimbia El Fasher zawasili Tawila.

© UNICEF/Mohammed Jamal

Familia nchini Sudan ambazo zimekimbia El Fasher zawasili Tawila.

Uchunguzi wafichua uhalifu mkubwa wa kivita

Uchunguzi uliofanywa na Ujumbe Huru wa Umoja wa Mataifa na ule wa ACHPR umebaini kuwa pande zote mbili pamoja na washirika wao zinahusika na ukiukwaji mkubwa, ikiwa ni pamoja na mauaji, mateso, kuzuia watu kiholela na mashambulizi yasiyochagua walengwa.

Mashambulizi ya anga, makombora na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani au droni katika maeneo yenye watu wengi yameripotiwa, huku miundombinu muhimu kama hospitali na masoko ya chakula ikilengwa, hali inayozidisha mgogoro wa kibinadamu uliokwisha kuwa katika hali mbaya.

Misaada ya kibinadamu yakwamishwa, wahudumu washambuliwa

Umoja wa Mataifa na AU pia wameeleza kuwa juhudi za kutoa msaada wa kibinadamu zimekuwa zikikwamishwa mara kwa mara, ikiwa ni pamoja na mashambulizi dhidi ya misafara ya misaada.

Wahudumu wa afya, wafanyakazi wa misaada na watetezi wa haki za binadamu wameuawa, kujeruhiwa au kuzuiliwa.

Aidha, mashambulizi ya kulipiza kisasi yanaendelea, huku pande zote zikilenga watu wanaodhaniwa kuwa wanaunga mkono upande pinzani.

Magari yaliyoteketea mjini Khartoum yanaonyesha jinsi mzozo huo umeathiri maisha nchini Sudan.

© Avaaz/Giles Clarke

Magari yaliyoteketea mjini Khartoum yanaonyesha jinsi mzozo huo umeathiri maisha nchini Sudan.

RSF yatuhumiwa kwa mashambulizi ya kimfumo na ukatili wa kijinsia

Kwa mujibu wa uchunguzi, ukiukwaji unaofanywa na RSF umeonekana kuwa wa kimfumo zaidi, ukiwemo uporaji, ukatili wa kijinsia na mashambulizi ya kikabila.

Katika tukio la kutekwa kwa mji wa El Fasher mwaka 2025, kulibainika mtindo wa kulenga makundi ya Zaghawa na Fur kwa misingi ya utambulisho wao, hali inayobeba viashiria vya mauaji ya kimbari.

Wito wa hatua za haraka na uwajibikaji

Kwa mujibu wa takwimu za Mashirika ya Umoja wa Mataifa zaidi ya watu milioni 8.6 wamekimbia makazi yao ndani ya nchi na wengine zaidi ya milioni 4 wamekuwa wakimbizi kufikia Machi 2026, huku wanawake na watoto wakibeba mzigo mkubwa wa mgogoro huo.

Mashirika hayo yametoa wito wa hatua za haraka, ikiwemo kusitishwa kwa mapigano, kuruhusu misaada kufika bila vikwazo, kuheshimu sheria za kimataifa na kuwajibisha wahusika wa uhalifu. Pia yamesisitiza umuhimu wa kuunga mkono juhudi za Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC na kuanzishwa kwa mifumo huru ya kisheria ili kuhakikisha haki inapatikana na amani ya kudumu inarejeshwa nchini Sudan.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *