Vizuizi na ukosefu wa usalama unaoendelea vimezidisha hali mbaya, vikizuia upatikanaji wa chakula, makazi salama na huduma za afya, na kuwaweka wanawake na wasichana katika hatari zaidi ya ukatili.
Kupitia mashirika yanayoongozwa na wanawake, UN Women inasaidia wanawake walio mstari wa mbele katika juhudi za kibinadamu na amani, kwa kutoa msaada wa kuokoa maisha na kutetea amani.
Wanawake ambao wamekimbia makazi yao wanapewa usaidizi huko Kassala, mashariki mwa Sudan.
Nini kinaendelea Sudan, na kinaathirije wanawake na wasichana?
Tarehe 15 Aprili 2023, vita vilizuka kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), vikisababisha janga kubwa zaidi la kibinadamu duniani kwa sasa. Tangu wakati huo, mzozo umeenea kote nchini, huku wanawake na wasichana milioni 17.1 wakihitaji msaada.
Vita hivi vimeambatana na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na ufurushwaji Mkubwa wa watu, ambapo wanawake na wasichana wameathiriwa zaidi.
Wamekumbwa na ukatili wa kutisha, ikiwa ni pamoja na ubakaji na aina nyingine za ukatili wa kijinsia majumbani mwao, wakati wa kukimbia, kambini, na wanapotafuta huduma muhimu. Ubakaji umetumika kama silaha ya vita.
Vizuizi na hali ya kutokuwa na utulivu vimewakatisha wanawake na wasichana kupata huduma muhimu, misaada ya kibinadamu na mahitaji ya msingi, huku wale walio katika maeneo yasiyofikika wakikabiliwa na hatari kubwa ya kifo na njaa.
Pia wanabeba mzigo mkubwa wa kulea familia, kulinda watoto na kutafuta chakula na maji katika mazingira hatarishi.
Hatari zipi zinazowakabili wanawake na wasichana?
Mamilioni ya wanawake na wasichana wamekimbia makazi yao kutokana na vita, wakikabiliwa na hatari kubwa wanapotafuta usalama. Kufikia mwaka wa nne wa mzozo, wanawake na wasichana milioni 4.3 bado wamekimbia ndani ya nchi, huku wengine wengi wakikimbilia nchi jirani.
Ufurushwaji huu unawaweka katika hatari ya ubakaji, utekaji nyara, ukatili wa kijinsia na hata kifo wanapotafuta chakula, maji na huduma za afya. Pia hulengwa katika makazi yenye msongamano mkubwa.
Wengi hulazimika kukimbia mara kwa mara huku wakiwajibika kuwahudumia watoto na wazee katika mazingira magumu.
Mfano, Khadija, aliyekimbia makazi yake Al Jazirah, alilazimika kurudi nyumbani wakati wa mapigano kutokana na maisha magumu uhamishoni. “Hatukuwa na chakula wala maji… hali ilikuwa ngumu sana,” anasema.
Khadija anaosha mboga nyumbani kwake katika mji wa Al-Waha, Madani, jimbo la Al Jazirah. Miaka miwili iliyopita, yeye na familia yake walikimbia kutoka nyumbani kwao huko Al Jazirah wakati mapigano yalipopowafikia.
Kwa nini wako katika hatari kubwa ya ukatili wa kingono?
Ubakaji na ukatili wa kijinsia umetumika kwa utaratibu kama mbinu ya vita Sudan. Wanawake na wasichana hulengwa majumbani, wakati wa kukimbia, na wanapotafuta huduma.
Vitendo hivi hutumiwa kutisha jamii, kudhalilisha na kuvunja mshikamano wa kijamii. Ndani ya miaka miwili ya kwanza ya vita, mahitaji ya huduma kwa waathirika wa ukatili wa kingono yaliongezeka karibu mara tatu.
Ingawa ukatili wa kingono umepewa kipaumbele katika simulizi za kimataifa, mchango wa wanawake katika kutoa msaada mstari wa mbele haujatambuliwa vya kutosha. Wanatoa huduma muhimu katika maeneo ambayo mashirika ya kimataifa hayawezi kufika, huku wakihatarisha maisha yao.
Ukosefu wa uwajibikaji kwa wahalifu na hofu ya unyanyapaa pia huzuia waathirika kuripoti matukio.
Kwa nini hawawezi kupata misaada ya kibinadamu na huduma za msingi?
Wanawake na wasichana wengi wamekatishwa kupata huduma muhimu kutokana na mapigano, vizuizi na ukosefu wa utulivu. Hali hii imeathiri upatikanaji wa chakula, maji, huduma za afya na ulinzi.
Vizuizi na kuzingirwa pia vimetumika kimkakati, na kuongeza mahitaji ya msaada. Mwaka 2026, wanawake na wasichana milioni 17.1 wanahitaji msaada, wakiwemo wajawazito milioni 1.1.
Sudan inakabiliwa na viwango vya juu vya ukosefu wa chakula, huku hatari ya njaa kali ikiendelea katika maeneo ya Darfur na Kordofan. Wanawake milioni 13.6 wanahitaji msaada wa chakula na maisha.
Wengi hulazimika kuchagua kati ya njaa au kuhatarisha maisha yao wakitafuta chakula.
Wanawake wanachukua nafasi gani katika mwitikio wa kibinadamu?
Wanawake wa Sudan wanaongoza juhudi za kibinadamu, wakitoa chakula, huduma za afya, msaada wa kisaikolojia na ulinzi kwa jamii zilizoathiriwa.
Pia wanashirikiana na makundi yenye silaha ili kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu na kulinda wanawake na wasichana dhidi ya ukatili.
Licha ya changamoto, wanaendelea kuendeleza jamii wakati mifumo rasmi imeporomoka.
Mfano, Amina, mkunga katika eneo la Darfur Kaskazini, hutoa huduma kwa wajawazito na watoto huku yeye mwenyewe akiwa mkimbizi. “Anatoa si tu huduma za afya bali pia matumaini.”
Amina ambaye ni Mkunga, anahudumia akina mama katika kituo cha afya kinachoungwa mkono na UNICEF huko Tawila, Darfur ya Kaskazini. Amina ni mhamiaji kutoka Al Fasher, na sasa anafanya kazi katika kituo hicho cha afya.
Ni changamoto zipi zinazokabili mashirika yanayoongozwa na wanawake?
Mashirika haya yanakabiliwa na ukosefu wa fedha, ukosefu wa usalama na vizuizi vya kufanya kazi.
Asilimia 99 ya mashirika yameripoti changamoto kutokana na upungufu wa rasilimali na vitisho vinavyotokana na mzozo. Mwaka 2025, asilimia 85 yalipungukiwa na ufadhili, na kusababisha kufungwa kwa huduma muhimu kama jikoni za jamii.
Wafanyakazi wanawake mstari wa mbele pia hulengwa moja kwa moja na vitisho vya ukatili.
Wanawake wanachangiaje juhudi za amani?
Utafiti unaonesha kuwa ushiriki wa wanawake huongeza uwezekano wa amani kudumu kwa asilimia 35. Hata hivyo, wanawake wa Sudan hawajashirikishwa kama wajadiliana katika mazungumzo rasmi katika miaka mitatu iliyopita.
Pamoja na kutengwa huko, wanaongoza juhudi za msingi za kujenga amani, kupunguza migogoro na kupinga kauli za chuki.
Ushiriki wao ni muhimu kwa amani ya kudumu na jumuishi.
UN Women inasaidiaje wanawake na wasichana?
UN Women hutoa msaada wa kuokoa maisha ikiwa ni pamoja na ulinzi, msaada wa kisaikolojia na vifaa muhimu.
Inashirikiana na zaidi ya mashirika 45 yanayoongozwa na wanawake katika majimbo 15 kufikia jamii zilizoathiriwa.
Pia inahamasisha uongozi wa wanawake katika maamuzi ya kibinadamu kupitia vikundi vya ushauri.
Mwanamke amebeba seti ya vifaa vya jikoni aliyopewa na shirika la UN Women Sudan kupitia Shirika la Sudanese Coalition for Education for All (SCEFA) katika eneo la mapokezi la Alazhri huko Port Sudan.
Wito wa hatua ni upi?
UN Women inataka:
- Kusitishwa mara moja kwa mapigano na ulinzi wa raia
- Ushirikishwaji kamili wa wanawake katika juhudi za kibinadamu na amani
- Uwajibikaji kwa wahalifu wa ukatili wa kijinsia
- Angalau asilimia 40 ya uwakilishi wa wanawake katika michakato ya amani
Miaka mitatu ya vita Sudan: Unachopaswa kujua
Ni mgogoro mkubwa unaoendelea, ukiendeshwa na vita, ukatili, njaa na ufurushwaji mkubwa wa watu, huku wanawake na wasichana wakikosa huduma za msingi na kuendelea kupambana kuishi.