Chanzo cha picha, EPA
Rais Donald Trump ameashiria kuwa mazungumzo yenye lengo la kumaliza vita nchini Iran huenda yakaanza tena wiki hii, baada ya majadiliano kuvunjika mwishoni mwa wiki iliyopita, jambo lililosababisha Marekani kuanzisha mzingiro wa bandari za Iran.
“Ningekushauri ubaki hapo [Islamabad], kwa kweli, kwa sababu kuna jambo linaweza kutokea ndani ya siku mbili zijazo, na tuna mwelekeo zaidi wa kwenda huko,” Trump alinukuliwa akisema katika mahojiano na New York Post.
Kauli zake zilikuja wakati jeshi la Marekani liliposema kuwa hakuna meli yoyote iliyopita katika mzingiro uliowekwa na Marekani kwenye bandari na maeneo ya pwani ya Iran katika saa 24 za kwanza za operesheni hiyo.
Mvutano huo umeibua mashaka kuhusu uwezekano wa kusitishwa kwa mapigano kwa muda wa wiki mbili ambako kunatarajiwa kumalizika wiki ijayo.
Upande wa Iran bado haujatoa majibu kwa kauli za Trump, lakini Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amesema kuwa kuna haja mazungumzo ya amani yarejee tena.
Maafisa kutoka nchi za Ghuba, Pakistan na Iran pia wamesema kuwa timu za mazungumzo kutoka Washington na Tehran zinaweza kurejea Pakistan baadaye wiki hii, ingawa tarehe rasmi bado haijakubaliwa, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.
Iran kwa kiasi kikubwa imefunga mlango bahari wa Hormuz, njia muhimu ya kimataifa ya usafirishaji wa mafuta na gesi, tangu iliposhambuliwa na mashambulizi ya anga ya Marekani na Israel tarehe 28 Februari.
Zaidi ya meli za kivita kumi na mbili za Marekani pamoja na takribani wanajeshi 10,000 wa Marekani sasa wanatekeleza mzingiro dhidi ya meli za nchi yoyote zinazoingia au kutoka katika bandari za Iran, hali inayonyima Iran chanzo muhimu cha uhai wa kiuchumi.
Pia unaweza kusoma: