Dar es Salaam. Benki ya Absa Tanzania imetangaza maboresho ya bidhaa yake ya Mkopo Binafsi Usio na Dhamana kwa wafanyakazi wa sekta binafsi na umma wanaopokea mishahara, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa mikopo nafuu na yenye masharti rafiki zaidi.
Kupitia maboresho hayo, kiwango cha juu cha mkopo kimeongezwa kutoka Sh150 milioni hadi kufikia Sh200 milioni, huku muda wa marejesho ukiongezwa hadi miezi 96, sawa na miaka nane, bila hitaji la dhamana.
Huduma hiyo inapatikana kwa wateja waliopo tayari wa benki hiyo pamoja na wateja wapya, kwa kuzingatia taratibu za tathmini ya uwezo wa mkopo.
Hatua hiyo inakuja kufuatia maboresho yaliyotekelezwa awali kwa wafanyakazi wa sekta ya umma, ambapo kiwango cha mkopo kiliongezwa hadi Sh200 milioni, muda wa marejesho kufikia miaka 10 na muda wa kusubiri nyongeza ya mkopo (top-up) kupunguzwa kutoka miezi sita hadi mitatu.
Mkuu wa Mikakati na Bidhaa za Wateja Binafsi wa Benki ya Absa Tanzania, Heristraton Genesis (kulia), akizungumza na waandishi jana jijini Dar es Salaam. Wengine kutoka kushoto ni Aron Luhanga, Mkurugenzi wa Masoko na Mahusiano na Ndabu Swere, Mkurugenzi wa Wateja Binafsi kutoka benki hiyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa maboresho hayo, Mkurugenzi wa Wateja Binafsi wa Absa Tanzania, Ndabu Swere, amesema benki hiyo imejikita katika kuelewa mahitaji ya wateja wake katika hatua mbalimbali za maisha yao ya kifedha.
“Tunatambua kuwa kila mteja ana safari yake ya maisha yenye mahitaji tofauti. Maboresho haya yanalenga kuwawezesha wateja kusonga mbele kwa kujiamini, iwe ni katika uwekezaji, makazi, elimu au mahitaji mengine muhimu,” amesema.
Ameongeza kuwa kuongezwa kwa kiwango cha mkopo na muda wa marejesho kunatoa unyumbufu kwa wateja kusawazisha majukumu ya sasa na mipango ya baadaye bila kubeba mzigo mkubwa wa kifedha.
Kwa mujibu wa Swere, wateja waliopo wanaokidhi vigezo wanaweza pia kuomba nyongeza ya mikopo au kufanya marekebisho ya mikopo yao (refinancing) kulingana na sera za benki.
Maboresho hayo yanaenda sambamba na kampeni ya “Jisogeze na Mkopo wa hadi TZS 200m”, inayolenga kuwahamasisha wateja kutumia fursa hiyo kujenga mustakabali wao wa kifedha.
Wateja wanaohitaji huduma hiyo wanashauriwa kutembelea matawi ya Absa, kuwasiliana na maafisa mahusiano au vituo vya huduma kwa wateja kwa maelezo zaidi.