Chanzo cha picha, Getty Images
Marekani imesema inajadili uwezekano wa kufanyika duru ya pili ya mazungumzo ya kutafuta amani na Iran.
Gazeti la Wall Street Journal limeripoti kuwa pande hizo mbili zimefikia makubaliano ya awali ya kukutana tena, ingawa muda na mahali pa mkutano huo havijabainishwa. Hata hivyo, Tehran imesema kuwa “misimamo ya Marekani inayobadilika na kukinzana inafanya kuwa vigumu kudumisha uaminifu wa makubaliano yoyote.”
Msemaji wa Ikulu ya White House amekanusha taarifa kwamba Marekani iliomba kurefushwa rasmi kwa usitishaji mapigano na Iran, akisema madai hayo “si ya kweli.”
Caroline Leavitt amesema, “tunaendelea kushiriki kikamilifu katika mazungumzo haya,” na kuongeza kuwa mazungumzo hayo ni “ya kujenga na yanaendelea.”
Akijibu taarifa kuhusu uwezekano wa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani, Leavitt alisema: “Majadiliano haya yanaendelea, lakini hakuna jambo lililo rasmi hadi litakapotangazwa hapa Ikulu ya White House.”
Aliongeza kuwa iwapo mazungumzo yatafanyika, kuna uwezekano mkubwa yakafanyika katika eneo lile lile la duru ya kwanza, yaani Islamabad, mji mkuu wa Pakistan.
Leavitt pia alisema kuwa kutekeleza matakwa ya Donald Trump, ambayo aliyataja kuwa “wazi na yasiyo na utata,” kutakuwa “kwa manufaa ya Iran.”
Ujumbe kutoka Pakistan ukiongozwa na mkuu wa majeshi Asim Munir uko Tehran kama sehemu ya juhudi za upatanishi.
Duru ya kwanza ya mazungumzo iliyofanyika mwishoni mwa juma lililopita mjini Islamabad, ilifeli kufikia makubaliano yoyote ya kuumaliza mzozo wa Mashariki ya Kati uliozuka tangu mwishoni mwa mwezi wa Februari.
Soma zaidi: