
Katika taarifa yao ya pamoja, iliyotolewa mjini Geneva Uswisi wataalamu hao wamesema “tuna wasiwasi mkubwa kuhusu madai yenye kuaminika ya usafirishaji wa kimfumo wa wanawake na wasichana kwa ajili ya ukatili wa kingono.”
Wametoa wito kwa mamlaka kote duniani kuanzisha “uchunguzi kamili na wa uwazi” kuhusu madai hayo yanayodaiwa kudumu kwa miongo kadhaa na kuvuka mipaka ya kimataifa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, faili hizo zina “ushahidi wa kutisha wa mitandao ya usafirishaji haramu inayohusisha watu mashuhuri, wakiwemo wanasiasa, wanadiplomasia, wafanyabiashara wakubwa na wana zuoni.”
Mapungufu katika haki na ulinzi
Wataalamu hao wameikosoa vikali serikali na vyombo vya sheria, wakisema majibu yao yamekuwa “duni kabisa hayalingani na uzito na dharura ya uhalifu unaodaiwa.”
Wameonesha kushindwa kwa mara kwa mara kuzuia biashara hiyo haramu ya binadamu, kubaini wahanga na kuwafikisha wahusika mbele ya sheria, wakisema hali hiyo imeruhusu uhalifu huo kuendelea duniani.
“Kukosekana kwa uwajibikaji kunadumisha utamaduni wa ukwepaji sheria,” taarifa hiyo imesema, ikiongeza kuwa hali hiyo inaathiri zaidi wanawake na wasichana na kudhoofisha ulinzi wa haki za binadamu kimataifa.
Mifumo dume iliyokita mizizi yazidi kuchunguzwa
Zaidi ya uwajibikaji wa jinai, wataalamu hao wameeleza madai hayo kama ushahidi wa ukosefu wa haki wa kimuundo.
“Usafirishaji huu mkubwa wa watoto unaweka wazi ubaguzi uliokita mizizi na ukatili wa mifumo ya mfumo dume,” walisema.
Pia wamelaani “ugeuzaji wa miili ya wanawake na wasichana kuwa bidhaa na kunyanyaswa kikatili,” wakirejelea ripoti za vyombo vya habari na picha zinazoonesha ukubwa wa ukatili huo.
Athari za kudumu na za kuharibu maisha
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya ukatili wa kingono “unahatarisha na kuharibu utoto” na huacha athari za muda mrefu za kimwili, kisaikolojia na kijamii.
Wataalamu hao wameonya kuwa madhara kwa manusura yanaendelea kwa muda mrefu, yakigusa afya, maisha na mustakabali wao.
Wito wa haki inayomweka manusura mbele
Wakiweka wahanga katikati ya mjadala, wataalamu hao wametoa wito wa hatua zinazozingatia kiwewe na jinsia, ikiwa ni pamoja na huduma za afya, msaada wa kisaikolojia na mipango ya urejeshaji wa muda mrefu.
Wamesisitiza kuwa haki lazima iende zaidi ya kuwafikisha wahusika mahakamani na ijumuishe “fidia na haki stahiki kwa manusura” pamoja na mifumo ya uwajibikaji inayoheshimu utu na mahitaji yao.
Wajibu wa kuchukua hatua umechelewa sana
Wakati umakini wa kimataifa ukianza kupungua, wataalamu hao wametoa onyo la mwisho kwa mataifa“Lazima tuende zaidi ya taarifa za vyombo vya habari hadi hatua madhubuti. Mataifa yana wajibu wa kuchukua hatua, na wajibu huo umechelewa sana.”
Wamezitaka serikali kuhakikisha upatikanaji wa haki, kuweka adhabu kali zinazostahili, na kuchukua hatua za kuzuia kurudiwa kwa uhalifu huo, wakisisitiza kuwa uwajibikaji ni muhimu katika kupambana na ukatili wa kijinsia wa kimfumo.