Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, ametoa agizo kali kwa madereva wanaopaki nje ya stand ndogo ya Kaloleni kuhakikisha wanaingia ndani ya eneo rasmi la stand hiyo kwa ajili ya kupakia na kuanzisha safari zao, hatua inayolenga kurejesha utaratibu na nidhamu katika sekta ya usafirishaji.

Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi katika eneo hilo akiwa ameambatana na Kamati ya Usalama ya Wilaya, Kilakala amesisitiza kuwa ni wajibu wa kila mdau kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kuhakikisha huduma za usafiri zinatolewa kwa ufanisi na usalama.

Aidha, amewataka viongozi katika ngazi mbalimbali kuacha kuweka mbele maslahi binafsi na badala yake kuwatumikia wananchi kwa uadilifu na uwajibikaji, akieleza kuwa kufanya hivyo kutachochea maendeleo endelevu kwa jamii na Mkoa wa Morogoro kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Emmanuel Mkongo, amesisitiza umuhimu wa kusimamia haki na usawa kwa wananchi wote, akibainisha kuwa kila mtu anapaswa kunufaika na kazi halali anayoifanya bila vikwazo au upendeleo.

Hatua hizi zinatazamwa kama sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha mifumo ya usafirishaji mijini, kupunguza msongamano usio wa lazima, na kuhakikisha huduma bora zinapatikana kwa wananchi huku nidhamu ya matumizi ya miundombinu ya umma ikizingatiwa.

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *