Vilabu mbalimbali alivyowahi kuchezea tayari vimetoa salamu za pole, ikiwemo Salzburg, ambayo ndio alioanzia soka lake.

Kipa wa zamani wa Arsenal na Liverpool, Alex Manninger, amefariki dunia baada ya kupata ajali ya gari iliyohusisha treni nchini Austria.

Kwa mujibu wa taarifa, tukio hilo limetokea leo Alhamisi Aprili 16, 2026 katika jiji la Salzburg, ambapo gari lake liligongwa na treni alipokuwa akivuka reli majira ya saa 2:20 asubuhi.

Inaelezwa kuwa wahudumu wa kwanza wa uokoaji walifika haraka eneo la tukio na kumtoa Manninger ndani ya gari lake, ambalo lilikuwa limebuluzwa kwa umbali fulani baada ya kugongwa. Madaktari wamejitahidi kumuokoa maisha yake, lakini kwa bahati mbaya hawakufanikiwa.

Ripoti zinaonesha kuwa Manninger alikuwa peke yake ndani ya gari, huku dereva wa treni pamoja na abiria takriban 25 wakiwa salama bila majeraha. Uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo bado unaendelea, ukihusisha kuchambua taarifa za kielektroniki za gari lake pamoja na hali ya taa za onyo kwenye kivuko cha reli.

Vilabu mbalimbali alivyowahi kuchezea tayari vimetoa salamu za pole, ikiwemo Salzburg, ambayo ndio alioanzia soka lake. Klabu hiyo imeeleza kushtushwa na tukio hilo na kutoa pole kwa familia na marafiki wa marehemu.

Manninger aliandika historia kwa kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Austria kucheza Ligi Kuu England alipojiunga na Arsenal mwaka 1997, ambapo alifanikiwa kushinda taji la ligi pamoja na Kombe la FA.

Baadaye aliwahi kucheza katika vilabu kadhaa barani Ulaya ikiwemo Juventus, ambako alitwaa ubingwa wa Italia (Scudetto), vilabu vingine alivyowahi kuvitumikia ni pamoja na Torino, Siena, Red Bull Salzburg, Udinese na Augsburg.

Rafiki yake wa karibu na gwiji wa soka wa Italia, Gianluigi Buffon, ametoa salamu za pile huku akieleza majonzi yake na kumtaja Manninger kama mtu wa kipekee aliyependa maisha rahisi nje ya soka.

Shirikisho la Soka la Austria pia limetoa salamu za pole, likimtaja marehemu kama balozi mzuri wa soka la nchi hiyo na mtu aliyekuwa mfano kwa makipa wengi chipukizi.

Manninger aliichezea timu ya taifa ya Austria mechi 33 kati ya mwaka 1999 hadi 2009, na alikuwa sehemu ya kikosi kilichoshiriki mashindano ya Euro 2008. Kifo chake kimeacha simanzi kubwa katika dunia ya soka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *