
Dar es Salaam. Unakumbuka ile Simba Day ya mwaka 2020 ambayo msanii Diamond Platnumz, alishuka na helikopta pale Uwanja wa Benjamin Mkapa na kutoa shoo kali?
Unaweza ukawa na historia ya tukio lenyewe, lakini usijue aliyekuwa nyuma ya kutengeneza wazo hilo na kulifanya likatimia, kisha kuacha histori kubwa.
Anaitwa Adam Kibaro, muandaaji wa tukio hilo ambalo liliacha historia kwa mashabiki wa Simba na Diamond pia kwa kuwa msanii wa kwanza kushuka na helikopta kwenye tukio kubwa kama hilo mwaka 2020.
Akizungumza na Mwananchi, Adam amesema, ni ngumu kwa waandaji kufahamika zaidi ya kazi zao, lakini yeye anaona fahari zaidi kufanya kazi nzuri ambazo zinaacha historia kubwa.
“Moja ya tukio la kihistoria ambalo sitakaa lisahaulike ni Simba Day ya mwaka 2020, ambapo msanii Diamond Platnumz aliingia uwanjani kwa kutumia helikopta. Muandaaji nilikuwa mimi na kampuni yetu ya AMOK Marketing Limited, ambayo imefanya mapinduzi makubwa ya kimasoko katika michezo nchini,” amesema Kibaro.
Ameongeza: “ Tuliikuta Simba Day ikiwa haina uwekezaji mkubwa wa branding, tukaingia na kufanya Simba Day ya kwanza ya mwaka 2020 ile ambayo Diamond Platnumz anaingia na helikopta uwanjani; Sisi ndio ambao tulifanya. Tumefanya kazi na Klabu ya Simba kwa miaka sita au saba sasa.
“Pia tumebadilisha namna ‘Trophy Handover Ceremonies’ (Sherehe za Makabidhiano ya Vikombe) zinatakiwa kufanyika kuanzia Ruangwa mpaka michuano ya kimataifa kama African Football League.
Amesema hata ile steji ambayo Alikiba anapanda na kombe linatoka, wametengeneza wao.
“Hakuna tukio kubwa la kimpira nchi hii ambalo limefanyika halijawahi kupita katika mikono yetu tangu 2019, zipo kama Azam Sports Federation Cup, NBC Premier League, na hata African Football League.
“Hivyo kabla ya kuingia kwenye tamthilia ambako nina miaka mitatu hadi sasa, nilikuwa na kampuni hiyo iliyojihusisha na kazi za ubunifu wa matukio mbalimbali.”
Kama wewe ni mfuatiliaji wa Tamthilia, basi unaijua ‘Koneksheni’ ambayo ilifanya vizuri na sasa ni ‘Noma’ ambayo inaendelea kufanya vizuri kupitia chaneli ya Sinema Zetu inayopatikana katika kisimbuzi cha Azam TV, hizo zote zimeandaliwa na Adam.