
Akizungumza na waandishi wa habari leo 16 Aprili katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amesema kuwa shirika hilo “liko tayari kuunga mkono juhudi hizi na linaendelea kusisitiza utekelezaji kamili wa Azimio la Baraza la Usalama namba 1701”. Azimio hilo linataka sitisho la kudumu la mapigano na suluhu ya muda mrefu ya mzozo huo.
Njia ya kufikia sitisho la kudumu la mapigano
Dujarric ameeleza kuwa azimio hilo linatoa mfumo wazi wa kufanikisha kusitishwa kwa mapigano kwa kudumu pamoja na suluhisho pana zaidi la kisiasa. “Utekelezaji kamili wa azimio 1701 unaelekea katika sitisho la kudumu la mapigano na suluhisho la muda mrefu kwa mzozo huu,” amesema.
Lililopitishwa mwaka 2006 kumaliza vita kati ya Israel na Hezbollah, azimio hilo linaweka masharti muhimu ikiwemo kusitishwa kwa mapigano, kuheshimiwa kwa msitari tenganishi kati ya Israel na Lebanon uitwalo Blue Line, na kuimarishwa kwa mamlaka ya serikali ya Lebanon kusini mwa nchi hiyo.
Juhudi za kidiplomasia zaendelea
Umoja wa Mataifa pia umethibitisha kuwa utaendelea na juhudi zake za kidiplomasia kati ya pande husika katika mzozo huo.
Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, Jeanine Hennis-Plasschaert, ataendelea na jukumu lake la kuleta maelewano na kusaidia utekelezaji wa makubaliano hayo.
Akisisitiza msimamo wa muda mrefu wa Umoja wa Mataifa, Dujarric ameongeza kuwa “hakuna suluhisho la kijeshi kwa mzozo huu,” akizitaka pande zote kuweka mbele diplomasia na kujizuia.
Matumaini ya tahadhari katika hali nyeti
Ingawa tangazo la sitisho la mapigano limeibua matumaini ya tahadhari, Umoja wa Mataifa umeonya kuwa msaada endelevu wa kimataifa na kikanda utahitajika ili kuhakikisha utulivu wa kudumu.
Shirika hilo limesema liko tayari kusaidia katika kuendeleza mazungumzo na kuhakikisha utekelezaji kamili wa Azimio 1701 unafikiwa.