Kupitia mahojiano hayo maalum, Bwana Tonderai Chikuhwa anaonya kuwa ukatili wa kingono ni jinamizi kubwa linalokumba wanawake na watoto nchini Sudan na umefika viwango vya kutisha, ukiathiri maelfu ya raia katika maeneo yote yaliyoathiriwa na mgogoro huo. 

Kwa masikitiko makubwa afisa huyo ameeleza kwa undani ukubwa wa janga hilo, mienendo yake, pamoja na madhara yake ya kijamii, kiafya na kiusalama kwa muda mfupi na mrefu akisema kuwa ukatili wa kijinsia nchini humo si tukio la nadra bali ni mbinu inayotumiwa kwa makusudi katika vita, ikilenga raia wasio na hatia katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

Bwana Tonderai anasema hali hiyo ni miongoni mwa masuala mabaya zaidi yanayoikumba Sudan kwa sasa..

“Tatizo hili la unyanyasaji wa kijinsia kutumika kama silaha ya vita ni moja ya masuala yenye uharibifu mkubwa na maumivu makali tunayokabiliana nayo. Ni jambo la kusikitisha sana kuona kinachowatokea raia nchini Sudan. Limeenea sana na linajitokeza katika kila eneo lililoathiriwa na mgogoro nchini Sudan, hivyo ni la kimfumo na linatumika kwa makusudi kama silaha ya vita.”

Mbali na madhara ya haraka kwa waathirika, Bwana Chikuhwa anaonya kuwa kuna athari nzito za muda mrefu, hasa kwa watoto wanaozaliwa kutokana na ukatili huo wa kingono.

“Ukitazama athari za muda wa kati na mrefu, kuna madhara makubwa ikiwa ni pamoja na tatizo la watoto wengi wanaozaliwa kutokana na unyanyasaji wa kijinsia wa wakati wa vita. Mara nyingi watoto hawa hukosa utambulisho kwa sababu ubaba hauwezi kuthibitishwa, huchukuliwa kama ‘watoto wa adui’ na hukataliwa na jamii. Hali hii inaweza kuwa chanzo cha migogoro ya baadaye na kupelekea vijana waliotengwa kujiunga na makundi yenye silaha.”

Umoja wa Mataifa unasisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za haraka kuwawajibisha wahusika na kulinda waathirika, huku ukionya kuwa bila hatua madhubuti, athari za mgogoro huu zitaendelea kwa vizazi vijavyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *