Akizungumza mjini The Hague Uholanzi, Guterres amekumbusha kuwa mahakama hiyo ilianzishwa baada ya Vita Kuu vya Pili vya Dunia kama sehemu ya juhudi za kujenga mfumo wa kimataifa unaotegemea sheria badala ya nguvu.
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa katika hotuba yake amesisitiza kuwa “nguvu ya sheria lazima ishinde sheria ya nguvu,” akieleza kuwa ICJ ni nguzo muhimu ya dunia yenye amani zaidi.
Kuhusu ICJ
ICJ, inayojulikana kama “mahakama ya dunia”, hushughulikia migogoro kati ya mataifa na kutoa ushauri wa kisheria kwa vyombo vya Umoja wa Mataifa.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Guterres, katika kipindi cha miongo minane iliyopita, maamuzi na ushauri wa mahakama hiyo yamechangia kuunda mfumo wa kisasa wa sheria za kimataifa.
Aliongeza kuwa ongezeko la mashauri yanayowasilishwa mahakamani hapo linaonesha imani ya mataifa katika uhuru na mamlaka yake.
Aidha, alieleza kuwa hatua za kuboresha utendaji wa mahakama pamoja na kuongeza uwakilishi wa kijinsia miongoni mwa majaji zinaonesha maendeleo muhimu katika kuifanya ICJ kuwa jumuishi zaidi.
Mahakama hiyo pia inaendelea kuhakikisha kuwa dhana ya mamlaka ya nchi na usawa wa mataifa si maneno matupu bali yanatekelezwa kwa vitendo kupitia sheria.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres anasaini kitabu cha kumbukumbu cha miaka 80 katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki huko The Hague.
Shinikizo kubwa
Akiendelea na hotuba yake Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa mfumo wa sheria za kimataifa uko chini ya shinikizo kubwa. Amesema ukiukwaji wa sheria hizo unaendelea kushuhudiwa, huku operesheni za kijeshi zikikiuka kanuni za msingi za vita na wajibu wa kibinadamu kupuuzwa. Aidha, taasisi za haki kama ICJ zinazidi kutiliwa shaka na hata kupingwa katika baadhi ya maeneo.
“Wakati sheria ya nguvu inapochukua nafasi ya nguvu ya sheria, migogoro huenea mipakani, mishtuko ya kiuchumi husambaa duniani, na walio dhaifu huathirika zaidi,” ameonya.
Guterres amesisitiza kuwa maamuzi ya ICJ, ikiwemo hatua za muda “provisional measures”, ni ya lazima kutekelezwa chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, na kuyaheshimu si chaguo bali ni wajibu wa kisheria kwa nchi zote wanachama.
Nini kinahitajika sasa?
Akihitimisha hotuba yake Katibu Mkuu Guterres aliwataka viongozi wa dunia kuzingatia mafuala yafuatayo.
- Kuchagua njia sahihi kwa kuimarisha sheria za kimataifa,
- Kutatua migogoro kwa njia za amani,
- Kufuata maoni ya ushauri ya mahakama
- Na kulinda misingi ya Umoja wa Mataifa.
“Katika wakati huu wa mgogoro, huu ndio uchaguzi sahihi pekee,” alisema, akisisitiza umuhimu wa kuwa na ujasiri wa kufanya uamuzi huo.