Dar es Salaam. Ni wazi kuwa Fatma Binti Baraka ‘Bi Kidude’ ni utambulisho wa muziki wa Zanzibar. Nyimbo zake kama Yalaiti, Muhogo wa Jang’ombe na nyinginezo zinaendelea kuishi masikioni mwa mashabiki wa muziki mzuri wa taarab na unyago.

Mkali huyo wa taarab hatimaye ametimiza miaka 13 tangu alipofariki dunia   Aprili 17, 2013 akiwa na umri wa miaka 103. Fahamu zaidi

Jina Kidude lilitokana na yeye kuzaliwa ‘njiti’. Ambapo jina hilo lilipata umaarufu zaidi kuliko jina lake halisi la Fatma.

Enzi za uhai wake Bi Kidude aliwahi kueleza kuwa alijifunza muziki kupitia mwanamuziki wa zamani aliyeitwa Sitti binti Saad. Hivyo kutokana na ukaribu uliokuwepo kati yao ikapelekea ajifunze kuimba Taarab.

Kwa kipindi hicho umahiri na umaarufu wa Sitti binti Saad kisiwani Zanzibar, ulipelekea wageni wengi waliofika kisiwani humo kupata shauku ya kutaka kumuona kila wanapotembelea kisiwa hicho kisha Bi Kidude alikuwa akiwapokea na kuwapeleka moja kwa moja kwa Sitti binti Saad.

Mbali na kuimba taarabu, Bi Kidude alikuwa mahiri katika ngoma ya unyago ambayo lengo lake ni kuwafunda wasichana ili kuelewa masuala ya ndoa na kuishi na waume zao vizuri.

Bi Kidude alikuwa maarufu mjini Zanzibar, lakini umaarufu wake ulivuka mipaka baada ya mwaka 1984 kufanyiwa mahojiano maalumu katika Televisheni Zanzibar na aliyekuwa Mkurugenzi wa televisheni hiyo, Abdallah Mwinyi Khamis.

Kama watoto wa kawaida alianza kuimba kwa sauti isiyo na mpangilio. Ilipofika mwaka 1920 alianza kuwa kinara wa kuimba na kucheza kwa ustadi ngoma ya unyago.

Bi Kidude alianza kuimba alipokuwa na umri wa miaka 10. Alianza kazi hiyo kwa kuburudisha katika majahazi yaliyokuwa yanachukua Waafrika na Waarabu katika Pwani ya Afrika Mashariki.

Uwezo wake mkubwa kwenye muziki wala haukuwa wa kificho  kwani ulimuwezesha kushinda tuzo mbalimbali kama ile ya mwaka 2012 ambapo alitunukiwa Tuzo ya ‘Michezo na Sanaa’ na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

Haikuishia hapo mwaka 2005 huko Gateshead, Newcastle nchini Uingereza, alitwaa tuzo ya heshima kutoka World Music Expo (WOMEX) na kuzawadiwa Euro 5,000.

Aidha alipata Tuzo ya Maisha ya Tamasha la Filamu la Nchi za Jahazi (ZIFF) mwaka 1999.

Sauti yake ilikuwa ikivuka mipaka kila kukicha na kumfanya atembelee nchi nyingi zikiwemo  Oman, Ufaransa, Hispania, Ujerumani, Uingereza. Katika sehemu zote alizokuwa anatumbuiza miguuni mwake alikuwa hana viatu ubunifu ambao unatumiwa na mwanamziki wa mashairi Mrisho Mpoto.

Enzi za uhai wake yapo matukio mengi yaliyowahi kutokea lakini lile la mwaka 2012 hukumbukwa na wengi. Baada ya Baraza la Sanaa Zanzibar kupiga marufuku kwa promota au muandaaji wa tamasha lolote kumsimamisha Bi Kidude jukwaani kutokana na afya yake.

Lakini mapenzi yake kwenye muziki yalijidhihirisha baada ya kukaidi kauli na kuonekana jukwaani akisalimia mashabiki wake kwenye tamasha la Sauti za Busara.

Hata hivyo, baada ya kusalimia alianza kuimba nyimbo kwa lugha ya Kiarabu na zile za unyago ambazo inasemekana yeye ndiye alikuwa akizitumia kuwafundisha mabinti wanaojiandaa kuolewa.

Tungo zake

Bi Kidude alikuwa gwiji katika muziki wa mwambao, alitunga, kuimba na kushiriki nyimbo nyingi akiwa na kikundi cha Culture Musical Club cha Zanzibar pamoja na vikundi mbalimbali.
Kati ya nyimbo zake maarufu ni Muhogo wa Jang’ombe ambao baadaye aliimba Judith Wambura ‘Lady Jaydee’, Msondo, Ahmada na Off side Trick, Kijiti, Uzuri wa Mwanaume si sura na Alaminadura.

Bila kusahau Yalaiti ambao  umekuwa ukirudiwa na baadhi ya wasanii akiwemo Mwana Fa na Esterina Sanga ‘Linah’
Iliwahi kuelezwa katika enzi za uhai wake, alionana na Malkia Elizabeth nyumbani kwake nchini Uingereza.

Asili yake

Enzi za uhai wake Bi. Kidude aliwahi kueleza maneno haya,
“Mimi asili yangu ni Mmanyema wa Kigoma, mama yangu alikuwa Mngindo, lakini baba yangu alilowea Zanzibar. Ndipo sisi tukazaliwa huko mpaka sasa naishi Zanzibar, lakini mie Mmanyema.”

“Enzi zetu taarab ulikuwa mtu ukiisikiliza ufanye kazi kupata maana. Kwanza, watu walikuwa wanaanza kuimba saa nane za usiku, ikifika saa 11 unafungwa muziki. Mimi nashangaa siku hizi taarab inaanza saa mbili,”aliwahi kusema Bi Kidude

Mkongwe huyo alizikwa katika Kijiji cha Kitumba, kilichopo Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *