Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Misitu nchini, Dkt. Tuli Msuya, amesema jumla ya miradi 137 imechaguliwa kunufaika na ruzuku kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kati ya zaidi ya maombi 400 yaliyowasilishwa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wanufaika wapya wa ruzuku hiyo, Dkt. Msuya alieleza kuwa kati ya miradi hiyo, 79 ni ya vikundi ambavyo baadhi yao tayari vimepatiwa mafunzo, huku wadau wengine 58 wakiendelea kupatiwa mafunzo hayo.

Alibainisha kuwa washiriki wa mafunzo hayo wanatoka katika sekta mbalimbali zikiwemo shule za msingi na sekondari, taasisi za serikali, taasisi za dini, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), pamoja na taasisi za utafiti na mafunzo.

“Lengo kuu la mafunzo haya ni kuwawezesha wanufaika wapya kutekeleza miradi yao kwa kuzingatia masharti ya mikataba ya ruzuku, kuhakikisha wanasaini mikataba ipasavyo, pamoja na kusimamia kwa ufanisi matumizi ya fedha wanazopokea,” alisema Dkt. Msuya.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa wanufaika kuandaa kwa umakini taarifa za maendeleo ya miradi pamoja na matumizi ya fedha ili kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwawezesha washiriki kuongeza ufanisi katika usimamizi wa miradi ya misitu, hatua itakayochangia katika uhifadhi na maendeleo endelevu ya rasilimali za misitu nchini.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa TAFORI, Dkt. Revocatus Mushumbusi, aliwataka wanufaika wa ruzuku hiyo kutumia vyema fursa waliyoipata kwa kuhakikisha wanajifunza na kuelewa kwa kina namna ya kusimamia miradi yao. Alieleza kuwa kutokana na idadi kubwa ya waombaji, waliopata ruzuku wanapaswa kuonesha uwajibikaji na ufanisi ili kuweza kunufaika zaidi na mfuko huo ambao ni endelevu.

Dkt. Mushumbusi aliongeza kuwa utendaji mzuri wa miradi hiyo unaweza kuwapa nafasi wanufaika kupata ufadhili zaidi katika siku zijazo, huku akibainisha kuwa hata taasisi yake ya TAFORI imenufaika na mpango huo na kupongeza juhudi za utoaji wa mafunzo hayo kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wa miradi.

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *