Tamasha la Family Day linaloandaliwa na Chuo cha Maafisa wa Polisi Tanzania – Kidatu kilichopo Mkoani Morogoro, limeendelea kuwa chachu ya kuimarisha uhusiano kati ya jeshi la polisi na jamii inayowazunguka kwani Kupitia tukio hilo, wananchi na askari hupata fursa ya kukutana katika mazingira ya kirafiki, hali inayochochea ushirikiano na kurahisisha juhudi za pamoja za kulinda amani na usalama.
Akizungumza wakati wa tamasha hilo, Mkuu wa Chuo hicho, SACP Zarau Mpangule, amesema kuwa Family Day imekuwa daraja muhimu la kuunganisha polisi na wananchi wa maeneo jirani, akieleza kuwa mahusiano hayo yameendelea kuimarika, na hivyo kuongeza uelewano unaohitajika katika kukabiliana na changamoto za kiusalama.
Kwa upande wake, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (Mkuu wa Idara ya Michezo) Amos Mikao amesema tamasha hilo limezaa matokeo chanya, hususan katika kuimarisha dhana ya ushirikishwaji wa jamii katika masuala ya ulinzi na usalama huku akibainisha kuwa ushirikiano huo umeongeza imani ya wananchi kwa jeshi la polisi na kuchochea uwajibikaji wa pamoja.
Aidha, Mikao amesisitiza umuhimu wa kuendeleza utamaduni wa michezo na matukio ya kijamii yanayowakutanisha polisi na wananchi kwani kupitia majukwaa hayo, hujengwa mshikamano, huimarishwa upendo, na kuwekwa msingi imara wa maendeleo endelevu yanayotegemea uwepo wa amani na utulivu katika jamii.
Tamasha hilo limepambwa na michezo mbalimbali ya kijamii na burudani, ikiwemo kukimbia na magunia, kubeba yai kwenye kijiko, kukimbiza kuku, kuvuta kamba pamoja na mpira wa miguu—michezo iliyoongeza hamasa, furaha na mshikamano miongoni mwa washiriki.
(Feed generated with FetchRSS)