
Munich, Ujerumani. Rekodi nane tofauti zimewekwa jana Jumapili, Aprili 19, 2026 wakati Bayern Munich ilipotwaa ubingwa wa 35 wa Ligi Kuu Ujerumani ‘Bundesliga’ baada ya kuichapa VfB Stuttgart kwa mabao 4-2.
Ushindi huo umeifanya Bayern Munich kufikisha pointi 79 ambazo ni 15 zaidi ya zile za Borussia Dortmund iliyo katika nafasi ya pili, jambo ambalo limeihakikishia ubingwa Bayern Munich kwa vile hata ikipoteza mechi nne ilizobakiza haiwezi kufikiwa kwa idadi ya pointi.
Kunogesha ubingwa huo, rekodi nane tofauti zimewekwa baada ya ushindi wa Bayern Munich jana.
Meneja wa Bayern Munich, Vincent Kompany anakuwa Kocha wa nane kushinda taji la Bundesliga katika msimu wake wa kwanza huku akiingia katika rekodi ya pili ambayo ni kuwa miongoni mwa makocha nane waliowahi kutwaa ubingwa huo katika msimu wao wa kwanza huku wakiwa hawajawahi kunoa timu katika Bundesliga hapo kabla.
Rekodi ya tatu ni Thomas Muller na Manuel Neur kuendelea kuwa mchezaji waliotwaa mara nyingi zaidi taji la Bundesliga ambapo kila mmoja amelibeba mara 13.
Bayern imeendelea kushikilia rekodi ya kuwa timu iliyotwaa mara nyingi zaidi taji la Bundesliga ambapo sasa imefikisha mataji 35.
Kipa Manuel Neur ameweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyeshinda idadi kubwa zaidi ya mechi za Bundesliga ambapo ushindi wa jana ni wa 368.
Kwa upande wa Thomas Muller, ambaye kwa sasa anacheza Vancouver ya Marekani, ameweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyepata ushindi mara nyingi zaidi kwenye Bundesliga akiwa na klabu moja ambapo ameshinda katika mechi 362 wakati akiwa na Bayern Munich.
Bayern pia imeendeleza rekodi ya kuwa timu iliyokusanya idadi kubwa ya pointi katika Bundesliga ikikusanya pointi 4,149 pia imeendeleza rekodi ya kuwa timu iliyopata ushindi katika mechi nyingi zaidi za ligi hiyo ikifikisha idadi ya michezo 1, 237.
Mabao ya Bayern Munich katika mechi ya jana yamefungwa na Raphael Guerreiro, Nicolas Jackson, Alphonso Davies na Harry Kane huku ya Stuttgart yakipachikwa na Chris Fuhrich na Chema Andres.