
Umoja wa Mataifan a Muungano wa Ulaya (EU) leo wametangaza kuwa gharama inayohitajika kujenga upya Ukanda wa Gaza imefikia dola bilioni 71.4, kufuatia karibu miaka miwili ya vita vilivyoacha miundombinu, uchumi na maisha ya kijamii katika hali mbaya sana.
Kupitia Tathmini ya Haraka ya Uharibifu na Mahitaji (RDNA) iliyofanywa kwa ushirikiano na Bank ya Dunia, taasisi hizo zimesema kiwango cha mateso ya binadamu na uharibifu ni kikubwa mno.
“Kiwango cha uharibifu na mateso ya binadamu huko Gaza hakijawahi kushuhudiwa,” ripoti hiyo imesisitiza.
Huduma muhimu zaporomoka, uchumi wadorora
Ripoti inaonesha kuwa dola bilioni 26.3 zinahitajika haraka ndani ya miezi 18 ya kwanza kurejesha huduma za msingi na kuanza ujenzi upya.
Sekta zilizoathirika zaidi ni pamoja na:
- Makazi: Zaidi ya nyumba 371,000 zimesambaratishwa au kuathirika
- Afya: Zaidi ya nusu ya hospitali hazifanyi kazi
- Elimu: Karibu shule zote zimeharibiwa au kuathirika
- Uchumi: Umeporomoka kwa asilimia 84
“Hili si tu janga la kibinadamu ni kuporomoka kamili kwa mifumo muhimu ya maisha,” imeeleza ripoti.
Uharibifu wa miundombinu pekee unakadiriwa kufikia dola bilioni 35.2, huku hasara za kiuchumi na kijamii zikifikia dola bilioni 22.7.
Maendeleo ya binadamu yamerudi nyuma kwa vizazi
Ripoti inaonya kuwa maendeleo ya binadamu Gaza yamerudi nyuma kwa takriban miaka 77.
Takribani watu milioni 1.9 wamekimbia makazi yao, wengi wao mara kadhaa.
“Zaidi ya asilimia 60 ya watu wamepoteza makazi yao,” ripoti inaeleza, ikiongeza kuwa wanawake, watoto na makundi yaliyo hatarini ndiyo walioathirika zaidi.
Amani na mwelekeo wa kisiasa ni muhimu
Ripoti inasisitiza kuwa ujenzi upya hauwezi kufanikiwa bila masharti muhimu ya kisiasa na kiusalama, yanayohusiana na Azimio 2803 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
“Sitisho la kudumu la mapigano na usalama wa kutosha ni masharti ya msingi. Bila hayo, hakuna ujenzi wala ukarabati unaoweza kufanikiwa,” Umoja wa Mataifa na EU wamesisitiza.
Masharti mengine muhimu ni pamoja na:
- Upatikanaji wa misaada ya kibinadamu bila vikwazo
- Uhuru wa kusafiri kwa watu na bidhaa
- Urejeshaji wa huduma muhimu
- Utawala ulio wazi na unaowajibika
Msisitizo wa uongozi wa Wapalestina katika ujenzi mpya
Mashirika hayo mawili yanasema ujenzi wa Gaza lazima uongozwe na Wapalestina, huku Mamlaka ya Palestina ikiwa na jukumu kuu.
“Ukarabati haupaswi tu kujenga upya yaliyoharibiwa, bali kuweka msingi wa mustakabali endelevu,” imeeleza ripoti.
Aidha, juhudi hizi zinahusishwa moja kwa moja na suluhisho la kisiasa,
“Maendeleo ya ujenzi wa Gaza, utekelezaji wa Azimio 2803, na suluhisho la mataifa mawili si mambo tofauti yamefungamana.” Imesema ripoti
Wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua haraka
Umoja wa Mataifa na EU zinatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka na zilizoratibiwa ili kupata fedha na kuondoa vikwazo vya ujenzi.
Vipaumbele ni pamoja na:
- Kuondoa vifusi
- Kudhibiti mabomu yasiyolipuka
- Kutatua migogoro ya ardhi na umiliki
“Jumuiya ya kimataifa lazima ichukue jukumu hili kwa uzito,” ripoti inahitimisha, ikiahidi kuendelea kuunga mkono “amani ya kudumu na ya haki.”
Wakati wa maamuzi makubwa
Wakati Gaza ikikabiliwa na gharama kubwa ya ujenzi inayofanana na uchumi wa baadhi ya nchi, ujumbe kutoka kwa taasisi za kimataifa ni wazi, “Wapalestina wanastahili mustakabali wenye heshima na haki ya kujitawala,” umesisitiza Umoja wa Mataifa na EU.