Wanablogu mashuhuri na watu wenye ushawishi kwenye mitandao ya kijamii wamekutana nchini Kenya na kuweka ahadi ya ‘Verify Before you Amplify’ yaani kuhakiki habari kabla ya kuzisambaza ili kulinda amani kuelekea uchaguzi mkuu wa nchi hiyo unaotarajiwa kufanyika mwaka 2027.
Mwenyekiti wa BAKE, Kennedy Kachwany ameeleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuimarisha ubora wa kazi zao ili kuongeza imani ya jamii kwao.
“Leo BAKE tumeanza mafunzo kwa watengeneza maudhui, na zaidi tunashughulika na watu ambao walishinda tuzo za BAKE mwaka jana au walikuwa miongoni mwa waliowania tuzo. Tunachofanya ni ufuatiliaji katika kujaribu kujenga kiwango cha ubora wa utengenezaji maudhui na pia kuwafanya watu hawa wawe sauti zinazoaminika zaidi tukiakisi baadhi ya changamoto tulizokutana nazo kuhusiana na baadhi maudhui.”
Watengeneza maudhui nchini Kenya waaswa kuwa walinzi wa amani na ukweli mtandaoni kupitia mafunzo yanayoendeshwa na UNESCO.
Misingi ya maadili na matumizi sahihi ya teknolojia mpya za kisasa imetajwa kuwa mhimili wa maudhui ya kimtandao. Anabainisha Mkufunzi na mtengeneza maudhui ya kidigitali, Rayhab Gachango.
“Tuko hapa kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo maadili, jinsi ya kutumia akili mnemba, AI kwa kuwajibika, na jinsi ya kuwa mtengenezaji bora wa maudhui.”
Mbali na maadili, Mtengeneza maudhui, Monicah Wangare anasema wamesisitizwa umuhimu wa uwazi katika kazi zao ili kujenga imani kwa hadhira inayowafuatilia kila siku.
“Kubwa zaidi kwangu imekuwa ni umuhimu wa kuweka wazi ikiwa video yako imedhaminiwa na watu fulani kwa kutumia alama, yaani hashtags, tangazo, au kuonesha kuwa umelipwa. Hii inaimarisha uaminifu wako kwa hadhira yako. Inajenga imani, na hiyo ni muhimu sana kwa yeyote ambaye ni nembo ya biashara”
Akielezea furaha ya kushirikiana na watengenezaji maudhui, Mratibu wa Programu kutoka UNESCO Kenya, John Okande amesema.
“Ni muhimu kwa watengenezaji maudhui ambao ni nguzo muhimu, kuhakikisha kuwa maudhui katika ulimwengu wa kidigitali kwanza yanakuza misingi ya haki za binadamu, pili yanaakisi muktadha wetu kupitia lugha mbalimbali tunazozungumza, na tatu yanajumuisha kila mtu.”