Akizungumza katika Mkutano wa 38 wa Kanda wa FAO NERC38 unaofanyika makao makuu ya shirika hilo mjini Roma, Italia Mkurugenzi Mkuu wa FAO, QU Dongyu, amesema mgogoro wa Mashariki ya Kati umefika katika “wakati muhimu” unaohitaji kulindwa kwa mtiririko wa biashara na kuhakikisha nchi zinazotegemea uagizaji zinapata chakula cha kutosha.

Mkutano huo unaoongozwa na Umoja wa Falme za Kiarabu UAE unawakutanisha mawaziri na watunga sera kujadili hatari zinazoongezeka kwa usalama wa chakula na mifumo ya kilimo. 

FAO imesema inaendelea kufuatilia athari za migogoro ya kimataifa ili kusaidia nchi wanachama kulinda mifumo yao ya chakula na maisha ya wakulima.

Athari zipo wazi tayari

Kwa mujibu wa FAO, mgogoro huo unasababisha kuvurugika kwa uzalishaji, biashara na usambazaji wa chakula, huku ukichochea kupanda kwa bei za nishati na mbolea, hali inayoongeza gharama za uzalishaji na kupunguza tija ya kilimo.

QU ameonya kuwa athari hizo zinaweza kudumu kwa muda mrefu hata kama mgogoro utaisha sasa, huku zikiathiri wakulima, wazalishaji na wadau wa minyororo ya thamani.

FAO imesisitiza kuwa amani ni sharti muhimu kwa usalama wa chakula, na mifumo imara na endelevu ya kilimo ni muhimu kwa kupunguza athari za migogoro na kuimarisha uthabiti wa jamii.

Mkutano huo umejadili pia hatua za kuimarisha minyororo ya usambazaji wa chakula, kuongeza uzalishaji wa ndani, kuwekeza katika miundombinu ya kilimo, na kuimarisha ushirikiano ili kukabiliana na changamoto zinazoikumba sekta hiyo.

Katika hatua nyingine ya kuhakikisha kuna upatikanaji wa chakula duniani soma hapa kuhusu Mawaziri wa Afrika aliokutana Nouakchott Mauritania kuharakisha mapambano dhidi ya njaa 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *