
Mwaka huu, kikao hiki, kimewakutanisha washiriki zaidi ya 1,000, wakiwemo Watu wa Asili, wawakilishi wa Nchi Wanachama, taasisi za Umoja wa Mataifa, na wasomi. Tadohaho Sid Hill Mkuu wa Jamii ya Onondaga amefungua kwa salamu za jadi, zikifuatiwa na hotuba kutoka kwa maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa, akiwemo Katibu Mkuu António Guterres; Rais wa Baraza Kuu Annalena Baerbock; Rais wa Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa, ECOSOC, Lok Bahadur Thapa; na Msaidizi wa Katibu Mkuu katika Idara ya Masuala ya Kiuchumi na Kijamii, Bjørg Sandkjær. Gavana Mkuu wa Canada, Mary Simon, pia amehutubia hafla ya ufunguzi. Yeye ni gavana wa kwanza wa Gavana kutoka jamii ya asili, Inuk.
Jukwaa la mwaka huu 2026 linaanza kazi zake huku wanawake wakichukua nafasi 11 kati ya 16 za wataalamu.
Lilianzishwa mwaka 2000, Jukwaa hili liloanzishwa mwaka limeweka masuala ya Watu wa Asili katikati ya mijadala ya kimataifa, likikuza utambuzi wa haki zao na kuimarisha ushiriki wao katika michakato ya kimataifa kwa kipindi cha miaka 25 iliyopita.
Mada ya mwaka huu inalenga kuhakikisha afya ya Watu wa Asili, ikiwemo katika muktadha wa migogoro, na inaangazia uhusiano wa karibu kati ya afya yao na ardhi zao, tamaduni zao na mifumo ya ikolojia, pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kama alivyobainisha Katibu Mkuu António Guterres, “Kwa Watu wa Asili, afya haiwezi kutenganishwa na ardhi zenu, maji, lugha, tamaduni na mifumo ya ikolojia.”
Licha ya kupitishwa kwa Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Watu wa Asili, maendeleo bado hayajasambaa kwa usawa, huku Watu wa Asili wakiendelea kukumbwa na ukosefu mkubwa wa usawa unaotokana na ukoloni na kutengwa kimuundo. Ingawa Watu wa Asili wanawakilisha takriban asilimia 6 ya idadi ya watu duniani, wanachangia karibu asilimia 19 ya watu wanaoishi katika umaskini uliokithiri.
Ukosefu huu wa usawa unaendelea kuathiri kwa kiasi kikubwa afya ya Watu wa Asili, hasa katika mazingira ya migogoro na majanga ya kimazingira. Wakati huo huo, vitisho dhidi ya viongozi wa Watu wa Asili na watetezi wa haki za binadamu vinaongezeka duniani kote. Taarifa zinaonesha kuwa takribani watetezi 196 wa ardhi na mazingira walipoteza maisha yao duniani mwaka 2023, wengi wao wakiwa Watu wa Asili. Katika muktadha huu, Mwenyekiti wa Jukwaa, Aluki Kotierk, anazitaka “Nchi kushughulikia ukiukwaji wa haki za binadamu kama jambo la kipaumbele, kuhakikisha haki na fidia kwa watetezi wa haki za binadamu wa Watu wa Asili walioathiriwa.”
Jukwaa hili si tu mahali pa kuangazia changamoto hizi, bali pia linakuza majadiliano, ushirikiano na suluu zinazoongozwa na Watu wa Asili, na linatumika kama jukwaa la kuimarisha mchango wao katika michakato ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa.
Aidha, Jukwaa litajadili masuala muhimu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na haki za binadamu na Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu. Pia litakuwa na mazungumzo ya haki za binadamu na Mtaalamu Maalum kuhusu haki za Watu wa Asili na Mfumo wa Wataalamu kuhusu Haki za Watu wa Asili, pamoja na Pendekezo la Jumla Na. 39 (2022) la CEDAW kuhusu wanawake na wasichana wa Asili. Majadiliano yataangazia pia ufadhili wa kazi na ushiriki wa Watu wa Asili katika mifumo ya kimataifa na kikanda, pamoja na kazi za baadaye za Jukwaa.
Katika kipindi cha wiki mbili za kikao, zaidi ya matukio 60 ya pembeni yataandaliwa na Nchi, Watu wa Asili na taasisi za kitaaluma. Katika wiki ya kwanza, eneo maalum la Vyombo vya Habari vya Watu wa Asili litatoa nafasi kwa vyombo hivyo kuripoti kikao hiki kwa lugha za Watu wa Asili. Maonesho yenye kichwa “Kutembea na Dunia: Watu wa Asili Wahamahama, Hekima ya Jadi, na Mustakabali wa Dunia” pia yataonyeshwa, pamoja na tukio la kitamaduni lililopangwa kufanyika Jumanne, tarehe 21 Aprili.
Idhaa hii ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa itafuatilia tukio hili kwa ukaribu ili kukuletea taarifa zaidi.